Saturday, August 8, 2020

Mgombea urais atinga kuchukia fomu akiwa na msafara wa bajaji


MGOMBEA Urais wa Chama cha Demokrasia Makini, Sesilia Mmanga ametinga na msafara wa bajaji katika Ofisi yaTume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC), kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya kuteuliwa kuwania nafasi hiyo.

Aidha, amesema katika kampeni za uchaguzi watatumia usafiri huo pamoja na pikipiki, baiskeli, guta na punda.

Mgombea huyo amefika katika ofisi hiyo akiwa ameambatana na Mgombea Mwenza wake Tabu Musa Juma na wanachama wengine kwa kutumia bajaji tatu na kukabidhiwa fomu na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mstaafu Semistocles Kaijage.

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa fomu, Mmanga amesema wananchi na wakulima wa hali ya chini usafiri wao ni wa bajaji.

“Chama chetu ni Demokrasia Makini yaani maana ya Makini ni Maarifa, Kilimo na Nishati, tumekuja na usafiri wa bajaji na bodaboda ili kuudhihirishia umma watakaponiteua mimi kama mama, wengi wananiita mama ushauri au mama THT, mama wa vipaji, hatutawabagua hata wale wa hali ya chini, tumekuja kivingine ili kuleta mabadiliko,”amesema.

Mgombea huyo amesema katika kampeni zao watatumia usafiri huo pamoja na guta, baiskeli na punda kwa kuwa wakulima wengi wanatumia baiskeli na punda ndo mbeba mizigo.

“Kwasababu chama chetu ni kikubwa na wakulima ni wengi tumejipanga, Demokrasia makini ni kubwa na tupo makini kama chama chetu, hatutalala kwa kuwa ukilala nchi inauzwa na sisi hatutaki nchi iiuzwe,”amesema.



source http://www.bongoleo.com/2020/08/08/mgombea-urais-atinga-kuchukia-fomu-akiwa-na-msafara-wa-bajaji/

No comments:

Post a Comment