Saturday, August 15, 2020

Jaji Kaijage amewaomba viongozi wa dini kuhubiri amani na wagombea kufuata sheria

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu wa Mahakama ya Rufaa, Semistocles Kaijage, amewaomba viongozi madhehebu ya dini mbalimbali kuhubiri amani na kuwasisitizia wagombea wa vyama vya siasa kuheshimu, kutii na kuzingatia sheria za nchi na kanuni za tume katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28, mwaka huu.

Ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam katika mkutano wa NEC na viongozi wa dini kuhusu Uchaguzi Mkuu.

Amesema NEC inatarajia wiki ijayo kukutana na wadau kujadili nafasi zao kama viongozi katika kufanikisha uchaguzi.

“Tutasimamia uchaguzi kwa kuzingatia Katiba, sheria na kanuni ili uwe huru, wa wazi na haki, wakuaminika na kuweka ushindani wa vyama vyote vinavyoshiriki,”

Amewaomba viongozi wa dini kuhimiza kampeni zitakazofanyika ziwe za kistaarabu na zenye kuepuka vitendo vya uvunjifu wa amani ya nchi.
Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum, amesema viongozi wa dini wana nafasi kubwa katika eneo la amani.

“Wananchi ni waumini wetu katika misikiti na makanisa, yaliyozungumzwa na Mwenyekiti wa Tume tunapaswa kuyachukua na kuwaeleza waumini namna bora ya kushiriki Uchaguzi Mkuu kwa kufuata nidhamu na taratibu,” amesema.

Mchungaji wa Kanisa la Moravian Tanzania, Jimbo la Mashariki, Neema Kashiririka, amesema ni vizuri viongozi wa dini wawaelekeze waumini umuhimu wa amani kwa sababu inapokuwapo watachagua kiongozi mzuri.



source http://www.bongoleo.com/2020/08/15/jaji-kaijage-amewaomba-viongozi-wa-dini-kuhubiri-amani-na-wagombea-kufuata-sheria/

No comments:

Post a Comment