Saturday, August 8, 2020

Takukuru yabaini ubadhirifu ujenzi wa ofisi za Wilaya

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imebaini ubadhirifu katika ujenzi wa Ofisi zake Wilaya ya Mpwapwa,Chamwino, Manyoni na jengo la Intelijensia lililopo Mkoani Dodoma.

Ubadhirifu huo umebainika baada ya kutekeleza agizo la Rais Dk.John Magufuli amelitoa Wilayani Chamwino wakati akifungua jengo la Ofisi hiyo ambalo aliagiza kufanyika upya kwa tathimini ya gharama za ujenzi zilizotumika kwenye majengo Saba kutokana na gharama zilizotumika kutoendana na majengo husika.

Akizungumza leo katika ufunguzi wa jengo la Ofisi ya TAKUKURU wilayani Mpwapwa,Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru brigedia Jenerali John Mbungo, amesema wahusika wote watachukuliwa hatua za kinidhamu na kufikishwa mahakamani.

Amefafanua kuwa katika kutekeleza agizo la Rais waliunda Tume iliyohusisha watu kutoka Mamlaka mbalimbali za nje na kuwapa siku saba za kufanya kazi hiyo.

“Jana Agosti 7 tume hiyo imenikabidhi taarifa iliyoonyesha kuwa baadhi ya wahusika kwenye ujenzi huo walikuwa na migongano ya kimaslahi hivyo watachukuliwa hatua za kinidhamu na kufikishwa mahakamani,”amesema.

Mbungo amesema taasisi hiyo ipo imara na itaendelea kuwa imara katika kuzuia na kupambana na vitendo vya rushwa hususani kipindi hiki Cha uchaguzi na kusema kamwe haitakuwa pango la wezi.



source http://www.bongoleo.com/2020/08/08/takukuru-yabaini-ubadhirifu-ujenzi-wa-ofisi-za-wilaya/

No comments:

Post a Comment