Wednesday, August 12, 2020

Shahidi asimulia alivyohama nyumba kisa meno ya tembo

MMILIKI wa Kituo cha kulelea watoto wenye usonji,Shabani Gweli ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa alihama nyumba aliyokuwa amepanga baada ya kukutwa na meno ya tembo.

Gweli ambaye ni shahidi wa saba katika kesi inayowakabili maofisa wa polisi wanne wa kituo cha Polisi cha Kawe mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Rashidi Chaungu.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Maghala Ndimbo alidai Februari mwaka 2018, aliingia mkataba na familia ya watoto wanne akiwemo Diana Naivasha, wa kupanga nyumba kwa ajili ya kuendesha kituo hicho kwa miaka mitatu na kwamba alitakiwa kulipa Dola za Marekani 4,000 kila mwezi.

Alidai ilipofika Septemba Mosi, 2019 alihama katika nyumba hiyo kwa sababu
watu mbalimbali wa serikali walikuwa walifika katika kituo hicho kwa ajili ya kufuatilia meno ya tembo yaliyokamatwa katika nyumba hiyo, jambo ambalo lingesababisha kukosekana kwa amani Kwa watoto waliokuwa wakiishi hapo.

Gwela ambaye ni mfanyabiashara alidai makubaliano mengine waliyoingia ni kwamba hakuruhusiwa kuingia chumba cha stoo kwa sababu kuna vitu ambavyo vimehifadhiwa hivyo, walifunga mlango na kuondoka na funguo.

“Aprili 13, 2018 alipigiwa simu ikielezea kwamba kwenye nyumba hiyo kuna meno ya tembo. Baada kukutwa kwa meno ya tembo, Askari polisi wa kituo cha Polisi Kawe, Shaban Shillah alinipigia simu na kunieleza ananiomba afike kituoni kwa ajili ya kufahamiana na kujua kituo changu nilichokuwa nikikiendesha,” alidai shahidi huyo.

Pia alidaiApril 14 mwaka 2019 alipigiwa Simu na ofisa wa Takukuru Kwa ajili ya mahojiano na April 15 mwaka 2019 aliombwa apeleke kitabu cha wageni cha maudhurio na mikataba ya pango la nyumba.

Baada ya kueleza hayo, Hakimu Chaungu aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 26, mwaka huu kwa kusikilizwa.

Washitakiwa katika kesi hiyo ni Shabani Shillah, Joyce Kita, Ulimwengu Rashid na Emanuel Njegele ambao wanadaiwa kuomba rushwa ya Sh milioni 200 kutoka kwa Naivasha.

Inadaiwa kuwa Desemba 17, 2018 eneo la Social Club Rainbow Kinondoni washtakiwa hao kwa pamoja wakiwa Maofisa wa Upelelezi walishawishi rushwa ya Sh milioni 200 kwa Naivasha wakidai amekamatwa na Nyara za Serikali ili kushawishi hatua za kisheria zisichukuliwe wanamsaidia.

Katika kosa jingine la kujihusisha na miamala ya rushwa kwa pamoja wanadaiwa Desemba 17, 2019 katika Kituo cha Polisi cha Kawe jijini Dar es Salaam waliomba rushwa ya Sh6 mioi kutoka kwa Naivasha kama kishawishi cha kumsaidia asichukuliwe hatua za kisheria baada ya kukamatwa na nyara za Serikali.

Katika kosa la nne, tano na sita ya kujihusisha na rushwa inadaiwa walilitenda Desemba 19, 2018 , Desemba 23, 2018, Januari 3, 2019 washtakiwa hao wakiwa Kituo cha Polisi cha Kawe na sehemu ya chakula Mgahawani kama waajiriwa katika nafasi zao walipokea sh 2 milioni kutoka kwa Naivasha kama kishawishi cha rushwa kwa madai anajihusika na nyara za Serikali.

Katika kosa la kughushi nyaraka linamkabili Joyce ambapo anadaiwa alitenda kosa hilo Desemba 2018 na Aprili 3, 2019 katika maeneo ya Kinondoni akiwa kama mwajiriwa wa Polisi kwa lengo la kudanganya alitengeneza nyaraka za uongo kwa jina la Naivasha akidai nyaraka hizo ni za kweli na zimewekwa sahihi na Diana wakati wakijua si kweli.

Pia wanadaiwa kutotii amri halali ya Ofisa wa Uchunguzi wa Takukuru ambapo inadaiwa Aprili 2019 wakiwa eneo la Baa Kinondoni wakiwa waajiriwa wa Polisi kwa pamoja walishindwa kutii amri halali ya kukamatwa ambayo ilitolewa na Mpelelezi wa Takukuru, Colman Lubisi.



source http://www.bongoleo.com/2020/08/12/shahidi-asimulia-alivyohama-nyumba-kisa-meno-ya-tembo/

No comments:

Post a Comment