Mkazi wa Manzese Argentina jijini Dar es Salaam, Asha Juma, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabili na mashtaka mawili ya kumiliki risasi 45 kinyume Cha Sheria.
Asha amefikishwa katika mahamakama hiyo leo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Agustina Mbando na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali Adolph Lema.
Katika shtaka la kwanza Lema alidai mshtakiwa huyo anakabiliwa na kosa la kumiliki risasi kinyume cha sheria ambapo ilidaiwa kuwa Mei 17, 2020 katika eneo la Manzese jijini Dar es Salaam alikutwa akimiliki risasi 29 zenye kipenyo milimita 12 kinyume cha sheria ya usimamizi wa silaha na risasi.
Katika shtaka la pili Asha pia anakabiliwa na kosa la kumiliki risasi kinyume cha sheria kosa analodaiwa kulitenda Mei 17, 2020 katika eneo la Manzese jijini Dar es Salaam, ilidaiwa kuwa alikutwa akimiliki risasi 16 zenye kipenyo cha milimita 9 kinyume na sheria ya usimamizi wa silaha na risasi.
Wakili Lema alidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika hivyo aliomba tarehe nyingine ya kutajwa.
Mshtakiwa hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina Mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo na alirudishwa rumande kwa kuwa mashtaka yanayomkabili hayana dhamana.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Agosti 26, 2020.
source http://www.bongoleo.com/2020/08/12/mwanamke-afikishwa-mahakamani-kwa-kukutwa-na-risasi-45-dar-es-salaam/
No comments:
Post a Comment