Monday, July 20, 2020

Waziri Ummy: Serikali imeandaa muongozi kuwapima Corona wanaotaka kwenda nje ya nchi

Serikali imesema anayehitaji huduma ya upimaji wa Covid-19 afike katika hospitali ya mkoa akiwa na uthibitisho wa uhitaji wa kupima kwa nchi anayotaka kwenda akiwa na hati ya kusafiria.

Kwa mujibu wa taarifa iiliyotolewa leo katika vyombo vya habari na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, imeeleza kuwa serikali imefungua anga lake ili kurejesha usafiri wa kawaida unaojumuisha ndege za biashara na abiria kwenda kwenye nchi mbalimbali.

“Kutokana na hali hiyo wizara imeandaa mwongozo wa kuwapima wasafiri wanaokwenda nje ya nchi hususani zile zenye hitaji la kupimwa maambukizi ya Covid-19. Mwongozo huu unalenga kuweka utaratibu wa upimaji wa wasafiri kwa hiari kwa wanaohitaji  kwenda kwenye nchi ambazo zinahitaji zinahitaji wawe wamepima kabla ya safari zao,” taarifa hiyo ilieleza.

Muongozo huo unaweka utaratibu wa maombi ya upimaji, namna ya kupata majibu, uhakiki mipakani na gharama za upimaji.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo imeeleza kuwa majibu ya vipimo yatatumwa kwa Mganga Mkuu wa Mkoa ambaye kwa wale ambao watakuwa hawana maambukizi watapewa vyeti. Majibu yatatolewa  ndani ya saa 72 . Wasafiri wote waliopewa vyeti majina yao yatatumwa mipakani kwa ajili ya uhakiki.

Gharama za vipimo kwa raia wa Tanzania ni Sh 40,000, Raia mkazi wa Tanzania ni Sh. 60,000 na raia wa kigeni ni Dola 100 za Marekani.



source http://www.bongoleo.com/2020/07/20/waziri-ummy-serikali-imeandaa-muongozi-kuwapima-corona-wanaotaka-kwenda-nje-ya-nchi/

No comments:

Post a Comment