Tuesday, July 28, 2020

Rais Magufuli atokwa na machozi akumbuka Mkapa alivyomsaidia, asema amepata pigo

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Magufuli, leo akihutubia Taifa wakati wa shughuli za mwisho za kuaga mwili wa Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, alimwaga machozi wakati akikumbuka ni kwa namna gani alikuwa akimsaidia wakati wa uhai wake na kuomba watu wasimshangae kisa analia.

Akitoa hotuba yake leo Rais Magufuli amesema mafanikio makubwa, yaliyopatikana kwa Taifa mara tu baada ya Rais Mkapa kuingia madarakani, ikiwemo suala la kukuza uchumi na kupunguza madeni ambayo nchi ilikuwa ikidaiwa na Mataifa pamoja na Mashirika ya nje.

Rais Magufuli amesema mzee Mkapa alimlea kama mtoto wake alikuwa ni shujaa wake na alimuonyesha upendo.

“Saa nyingine machozi yanakuja tu msinishangae hata mzee Kikwete nilimuona juzi akidondosha machozi tena Kikwete ni Kanali ila alitoa chozi kwa hiyo msinishangae wakati mwingine kifo hauwezi kukivumilia nasema kweli alinionyesha upendo mkubwa kuondoka kwake ni pigo kwangu,”

Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin William Mkapa, alifariki Dunia usiku wa kuamkia Julai 24, 2020, kutokana na tatizo la mshituko wa moyo na atazikwa siku ya kesho Julai 29, 2020, katika Kijiji cha Lupaso, Masasi mkoani Mtwara



source http://www.bongoleo.com/2020/07/28/rais-magufuli-atokwa-na-machozi-akumbuka-mkapa-alivyomsaidia-asema-amepata-pigo/

No comments:

Post a Comment