Habari ya asubuhi mdau wa Opera News ni siku nyingine ya Ijumaa Julai 31, 2020, matumaini yetu upo salama na karibu katika ujenzi wa taifa.
Tunakukaribusha katika dawati letu la dondoo tupate kukujuza habari tatu zinazopamba asubuhi ya leo.
Habari hizo ni Watu 10 wamefariki na wengine 100 kuokolewa katika ajali ya boti mkoani Kigoma, Kesi ya Lissu na mustakabali wake katika safari ya kuusaka Urais na Shahidi aeleza Diwani wa CCM alivyopokea rushwa na kukamatwa.
WATU 10 WAMEFARIKI NA WENGINE 100 KUOKOLEWA
Watu 10 wamefariki dunia na wengine 100 wameokolewa baada ya boti waliyosafiri nayo kupatwa dhoruba na kuzama katika ziwa Tanganyika.
Mkuu wa mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye amethibitisha kutokea kwa tukio.
KESI DHIDI YA LISSU, MUSTAKABALI WAKE KATIKA SAFARI YA URAIS
Siku chache baada ya kuwasili nchini Tanzania akitokea kwenye matibabu huko Ubelgiji na kulakiwa na maelfu ya wafuasi na wanachama wa Chadema, mwanasiasa Tundu Lissu ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa chama hicho ameanza kuonja joto la kesi zinazomkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi jijini Dar es salaam.
Suala hili limeibua hisia tofauti kuhusu hatima ya kiongozi huyo katika kinya’ng’anyiro cha urais ndani ya chama, muungano mwaka huu wa 2020 na siasa kwa ujumla, licha ya haki zake kulindwa na katiba kwa vile hajawahi kutiwa hatiani kati ya tuhuma zilizomkabili kwa kipindi cha miaka mitano.
SHAHIDI AELEZA DIWANI WA CCM ALIVYOPOKEA RUSHWA
SHAHIDI wa kwanza Yusufu Shaban Omar Matimbwa katika kesi inayomkabili Diwani wa Kijichi, Mbagala jijini Dar es Salaam Elias Mtarawanje (29), anayedaiwa kupokea rushwa, ameeleza namna Polisi walivyoweka mtego na kufanikiwa kumnasa kiongozi huyo wa Chama cha Mapinduzi (CCM).
Shahidi huyo ambaye ni mwekezaji wa Hotel ya Giraffe Temeke jijini Dar es Salaam, leo Alhamisi tarehe 30 Julai 2020 amedai ana ushahidi wa kutosha kuithibitisha mahakama kuwa Diwani huyo alipokea rushwa ya sh milioni moja za mtego kutoka kwake.
Diwani Mtarawanji alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke mwaka huu, akikabiliwa na mashtaka mawili likiwamo la kupokea rushwa ya Sh. 1 milioni kutoka kwa Matimbwa.
source http://www.bongoleo.com/2020/07/31/dondoo-za-leo-watu-10-wamefariki-na-100-waokolewa-kesi-ya-lissu-na-mustakabaliwake-katika-safari-ya-urais-na-shahidi-aeleza-diwani-wa-ccm-alivyopokea-rushwa/
No comments:
Post a Comment