Tuesday, July 28, 2020

Mwanafunzi Ajitia Kitanzi Baada ya Kutumwa Kuchuna Mboga Shambani

Babake msichana huyo alipigwa na bumbuazi kuupata mwili wa mwanawe ukining’inia mtini. Picha: Hisani

Mwili wake ulipatikana ukininginia kwenye mti shambani alikotumwa kuchuna mboga

Hakuacha ujumbe wowote kueleza kilichomplekea kuchukua hatua hiyo

Wenyeji katika kijiji cha Nyabwachche, Gwasi, Suba Kusini Kenya wamesalia kwa huzuni kubwa kufuatia kifo cha mwanafunzi mwenye umri wa miaka 15 aliyejiua kwa njia ya kutatanisha.

Kulingana na kisa hicho kilichofanyika Jumatatu, Julai 27, mwili wa Yvonne Atieno Nyamweya ulipatikana ukining’inia mtini nyuma ya nyumba yao.

Kwa mujibu wa chifu wa eneo hilo Tobias Opiyo, Yvonne alitumwa shambani kuchuna mboga na kuchukua muda mrefu kabisa kabla kurudi nyumbani, babake aliamua kuenda shambani alikotumwa kuangalia alichokuwa akifanya.

Maurice Nyamweya babake msichana huyo alipigwa na bumbuazi kuupata mwili wa mwanawe ukining’inia mtini.

Opiyo alieleza kuwa mwanafunzi huyo aliyekuwa katika darasa la saba kwenye shule ya Nyabwacheche hakuacha ujumbe wala andiko lolote kueleza kilimfanya kujitia kitanzi.

Aidha, alieleza kuwa mtoto huyo aliyekuwa akiishi na mama wa kambo hakuonyesha dalili zozote za msongo wa moyo kabla kuchukua hatua ya kujitia kitanzi.

Mwili wa mwendazake umepelekwa katika makafani ya Kirindo kusubiri upasuaji ili kubaini chanzo cha kifo huku polisi wakianzisha uchunguzi katika kisa hicho.

Chifu huyo amewashauri  wazazi kudumisha uhusiano mzuri na watoto na kuwapa ushauri kama njia ya kuwarudi na pia kuwawezesha kufunguka kuhusu shida wanazopitia.



source http://www.bongoleo.com/2020/07/28/mwanafunzi-ajitia-kitanzi-baada-ya-kutumwa-kuchuna-mboga-shambani/

No comments:

Post a Comment