Friday, July 24, 2020

“Baba Mkapa yule”

Ilikuwa ni mwaka 2000 katika viwanja vya Mkendo pale Musoma mjini, wakati huo nikiwa na miaka 7 niko juu ya mabega ya baba yangu katikati ya maelfu ya watu wakimuangalia msomi wa chuo cha Makerere, Mwanahabari wa gazeti la (Nationalist) Uhuru, Mwanadiplomasia makini na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Msomi huyu wa chuo kikuu cha Columbia akiwa viwanja vya Mkendo siku hiyo alikua na kazi moja tu ya kuomba ridhaa ya kuingia tena Magogoni na kuwapa mrejesho wananchi wa kile walichomtuma mwaka 1995.

“Baba, Mkapa yulee.” nilitamka manano haya nikiwa juu ya mabega ya Baba yangu ambaye alifanya jitihada za dhati kunifanikishia azma yangu niliyokuwa nayo ya kumuona mtu niliyekuwa nazisikia hotuba zake kwenye radio yetu ya National tukiwa mitaa ya Mwisenge na Kamnyonge pale Msoma mjini.

 

 

Mapenzi yangu ya dhati ya Chama Cha Mapinduzi yalizaliwa hapa rasmi kwani nilipendezwa na zile sare za kijani mithilii ya majani yaliyokatwa vyema kwaajili ya shughuli hii maridhawa pale Mkendo, nilivutiwa na sare zile kwasababu ya upendo wangu kwa Baba yangu ambae ni shabiki mkubwa wa wanajangwani.

Baba yangu licha ya kuwa ni mtumishi kwenye moja ya vyombo vya ulinzi na usalama nchini, nakumbuka nilimuomba anipeleke kumuona yule mtu mwenye sauti ya ushawishi iliyojaa mamlaka niliyokua nikiisikia redioni.
Baba alichukua baiskeli yake aina ya Swala iliyokuwa imerembwa vyema na huku nyuma ikiwa na ulimi uliokuwa umeandikwa “Mwega 2” Leo nataka nimuulize mzee sijui maana ya ili neno ilikua ni nini? Ha ha ha! Siku niliyomuona Ben ilizijenga fikra zangu na ndiyo iliyonitengenezea leo yangu na imani kubwa kwa kesho yangu.

Wakati tunarudi nyumbani na baisakeli yetu chapa SWALA tukiwa tunakatiza mitaa ya Nyasho njiani nilimuuliza Baba kuwa kabla Mkapa hajawa rais alikuwa nani? Mzee alinijibu kwa kusema aliwahi kuwa mwandishi wa habari gazeti la Nationalist (Uhuru).
Hapa ndipo nilianza safari yangu ya kuwa mwanadiplomasia na mwandishi wa habari na nilipenda sana kusikiliza radio haswa RTD pamoja na RFA na baedae Baba alinunua TV kubwa ya chogo chapa Hitachi. Basi bwana hapo ndio ikawa mimi na TVT, TVT na mimi!
Mwaka 2004 Baba yangu alihamishiwa Arusha pamoja nami na mdogo wangu Salma. Nikasoma Burka Primary, Elerai Secondary School, Winnings Spirit na masomo yangu ya Advance nilichukulia pale Mwanga Secondary School, shule kongwe ya Chama cha Mapinduzi.
Waliosoma na mimi shule zote hizo wanayajua vyema mapenzi yangu kwa Ben na Chama Cha Mapinduzi kwani ilifika mahali nilijifananisha naye. Badala ya Mrisho Selemani wakawa wananiita “Mkapa” na nilifanikiwa kushika nyadhifa mablimbali kuanzia shuleni hadi pale chuo kikuu cha Dar es salaam nilipokua nasomea shahada ya kwanza ya uandishi wa habari.


Hivi sasa nimekuwa Mwandishi wa habari Opera News  na mtaalamu wa masuala ya mitandao ya kijamii na najiendeleza kwa kusomea Masoko kwa ngazi ya cheti pamoja na Diplomasia kwa ngazi ya Uzamili, na yote ni kutokana na ushawishi niloupata kutoka kwa Ben.

Usiku wa tarehe 23 Julai mwaka 2020 ulikuwa ni usiku ambao sitokuja kuusahau katika Maisha yangu yote! Ni usiku ambao ulinitoa machozi sana, ni usiku ambao nilitami nizinduke kutoka ndoto nzito na kukaa kitako kitandani kwangu. Nilitamani kukataa kusikia kama sio kuelewa kile nilichokuwa nakisikia kwenye redio. Ben amefariki! Hapana,ilikuwa ni ngumu sana kwangu kuipokea taarifa hii. Nilibadilisha masafa ya redio ili nikutane na kitu kingine tofauti na hicho, lakini wapi! Taarifa ilibaki kuwa hiyo tu kwenye redio zote, Ben ametutoka.

Huu ni wakati mgumu sana kwa taifa,nafahamu, lakini kwangu mimi huu ni wakati mgumu maradufu! Kiigizo changu, mpendwa wangu, mtu niliyemchagua kuwa mfano kwangu nikiwa mabegani mwa baba yangu katikati ya mamia ya watu, mtu aliyenifanya leo hii mimi nimekuwa mwandishi wa habari, Rais Benjamin William Mkapa leo hatunaye tena? Itanichukua muda kulikubali hili na kulizoea.
Mungu ailaze mahali pema peponi roho ya mpendwa wetu, Benjamin William Mkapa. Amen.



source http://www.bongoleo.com/2020/07/24/baba-mkapa-yule/

No comments:

Post a Comment