Thursday, July 16, 2020

Lissu atema Cheche kwa kitendo cha jeshi la polisi kutaka majina ya wagombea Chadema

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maebdekeo (Chadema), Tundu Lissu amesema jeshi la polisi halina mamlaka na mchakato wa uteuzi wa wagombea.

Lissu ambaye alikuwa mbunge wa Singida Mashariki amesema Mkuu wa Polisi Wilaya ya Nzega Mayala amevuka mipaka ya mamlaka yake.

“Jeshi la polisi halina mamlaka wala jukumu lolote kuhusiana na mchakato wa uteuzi wa wagombea uchaguzi ndani ya vyama vya siasa au kwenye Tume ya Uchaguzi,” aliandika Lissu katika ukurasa wake wa Twitter.

Aliongezea kuwa “OCD Mayala amevuka mipaka ya mamlaka yake. Anastahili sio kukanywa tu, bali kuchukuliwa hatua stahiki za kinidhamu,”.

Mkuu wa polisi wa Wilaya ya Nzega amewaandikia barua Chadema ya kuwataka kuwasilisha majina ya watia nia katika majimbo ya Nzega mjini, Nzega vijijini na Bukene.

Barua hiyo ilieleza kuwa “Naomba kupatiwa majina ya watia nia kupitia chama cha Chadema kwa majimbo ya Nzega mjini, Nzega vijijini na Bukene majina hayo niyapate kabla ya tarehe 15/07/2020 kwa hatua zangu,”.

Barua hiyo ilianza kuzunguka katika mitandao ya kijamii na kusababisha mijadala wengine kuhoji tangu lini majina ya wagombea yakawasilishwa polisi.



source http://www.bongoleo.com/2020/07/17/lissu-atema-cheche-kwa-kitendo-cha-jeshi-la-polisi-kutaka-majina-ya-wagombea-chadema/

No comments:

Post a Comment