Wednesday, July 15, 2020

Mume amuua mkewe kwa kumchinja shingoni na yeye kujinyonga

Mkazi wa Kijiji cha Mipanga Kata ya Maji Moto Wilaya ya Mlele Mkoa wa Katavi, Dalali Malongo (20) ameuawa kikatili kwa kuchinjwa shingo na mume wake aitwaye, Kisabo  Joseph baaada ya mume wake kukasirishwa na kitendo cha mke wake kumnyima tendo la ndoa kwa muda mrefu.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Benjamin Kuzaga amesema tukio hilo la mauaji lilitokea Julai 14, mwaka huu majira ya saa moja jioni Kijiji cha Mipanga Kata ya Maji Moto Wilaya ya Mlele.

Amesema marehemu na mtuhumiwa walikuwa ni wanandoa waliokuwa wakiishi pamoja kama mume na mke.

“Katika ndoa yao inasemekana marehemu alikuwa akikataa kufanya tendo la ndoa pindi mume wake alipokuwa akihitaji kupatiwa tendo la ndoa na mke wake,” amesema kamanda.

Kamanda amesema inadaiwa marehemu huenda alikuwa na mahusiano na mwanaume mwingine ambaye alikuwa akifanya naye tendo la ndoa na kumnyima mume wake.

Amesema hali hiyo imesababisha mume wa marehemu achukie, hivyo siku ya tukio mume wake alimvizia marehemu wakati akienda kuteka maji kwenye chanzo cha Maji ya Moto.

Kamanda Kuzaga amesema, ndipo alipomvizia marehemu na kuchinja shingoni kwa kutumia kisu na kufariki.

Baada ya kutekeleza mauaji hayo ya mke wake, Kisabo Joseph naye aliamua kujinyonga juu ya mti kwa kutumia kamba na kufariki dunia jirani na aliko mchinjia mke wake.

Kamanda amesema upelelezi  wa awali wa tukio hilo wamebaini chanzo cha mauwaji hayo yamesababishwa na wivu wa mapenzi.

Aidha,  ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Katavi hasa kwa wanandoa  wawe na tabia  ya kushughulikia masuala yao kifamilia  kwa kuzingatia  mwenendo mwema wa taratibu za kijamii kwa kushirikiana na viongozi wa dini na wa kimila katika maeneo yao ili kuepukana na matukio ya namna hiyo ndani ya jamii.



source http://www.bongoleo.com/2020/07/16/mume-amuua-mkewe-kwa-kumchinja-shingoni-na-yeye-kujinyonga/

No comments:

Post a Comment