UKIFANYA tathimini za kina, utagundua mapenzi ni muhimu sana katika maisha yetu ya kila siku. Mapenzi ni kichocheo cha furaha, amani na mshikamano. Mapenzi yanaleta utulivu wa akili, yanatibu matamanio ya mwili.
Mapenzi yanaleta ufanisi wa kazi. Unapokuwa na ugomvi na mwenzi wako, ni dhahiri kwamba mambo yako mengine ikiwemo ya uzalishaji, yatayumba kama si kuharibika kabisa.
Hivyo basi, ukiyatathimini mapenzi kwa ujumla wake, yana faida nyingi lakini leo nataka nikuongee kitu kwennye ubongo wako, uaminifu ni muhimu zaidi kuliko hata mapenzi.
Uaminifu ni ngao ya mapenzi. Bila uaminifu hakuna mapenzi. Utampenda mtu sawa lakini bila uaminifu, mapenzi ni kazi bure. Mtaishi lakini mbeleni mtaishia kuachana. Mapenzi bila uaminifu ni sawasawa na na gari linalokwenda bila dereva.
Litaenda safari lakini itafika sehemu litaanguka. Uaminifu ni dira. Uaminifu unajenga tabia njema. Uaminifu ni silaha ya uhai wa penzi hivyo ni vyema mtu ukawa mwaminifu kwanza kabla hata ya kuingia kwenye mapenzi.
Uaminifu pia unaleta busara. Busara inawafanya wapendanao watatue matatizo yao kwa amani na utulivu. Busara inaepusha machafuko. Uaminifu ni msingi wa busara kama alivyosema muasisi wa madhehebu ya Buddha, Gautama Buddha:
“Honesty is the first chapter in the book of wisdom.”
Ukiingia kwenye mapenzi ukiwa huna uaminifu, ni sawasawa na kufuga bomu ndani ya nyumba. Matunda ya kutokuwa na uaminifu siku zote ni usaliti. Usaliti unaleta maafa. Usaliti unatengeza chuki, usaliti unavunja uhusiano au ndoa.
Marafiki zangu, dunia ya leo sisi wote ni mashahidi. Tunashuhudia matukio mengi sana ya usaliti yanavyogharimu maisha ya watu. Usaliti ndio unafanya watu wavunje ndoa au wasisemezane maisha yao yote.
Watu wanauana kwa sababu tu, uaminifu umevunjwa. Ndio maana nikasema, uaminifu ni mhumu kuliko hata mapenzi. Wazungu wanasema; “In a relationship, trust is more important than love. It will enhance your love.”
Uaminifu ndio unaoongeza au kujazia maana halisi ya mapenzi. Ni bora kabisa usiwe na mpenzi lakini uwe muaminifu. Maana, uaminifu una tija kubwa hata kwenye maisha ya kawaida. Unapokuwa muaminifu, wanaokuzunguka watakuamini na kukupenda.
Nikushirikishe pia na msemo huu wa Kingereza; “I trust you” is better than “I love you” because you may not always trust the person you love but you can always love the person you trust.”
Anaaminisha neno ‘nakuamini’, ni jema zaidi kuliko neno ‘nakupenda’ kwa sababu hatumuamini yule tunayempenda ila tunampenda yule tunayemuamini.
Ukiwa muaminifu hata kazini, utasikia wenzako wakisema, ‘napenda kufanya kazi na fulani kwa sababu ni muaminifu.’ Fulani anaaminika hata ukimkopesha, si msumbufu wa kulipa.
Uaminifu una manufaa makubwa kuliko kutokuwa nao. Uaminifu unakufanya uheshimike. Ukiwa muaminifu hata mawasiliano yako yatakuwa mazuri na mwenzi wako. Hamtagombana gombana. Mtaheshimiana. Uaminifu unaanza na wewe, ukiwa muaminifu, mwenzako naye atakuamini.
Jifunze kwa msemo huu: “When the trust is high, communication is easy, instant, and effective.” (Kiwango cha uaminifu kikiwa juu, moja kwa moja mawasiliano yenu yatakuwa mazuri.)
Ili maisha yaende, unashauriwa kujenga imani kwa mwenzako ili naye aweze kukuamini. Usiwe na mashaka naye. Mwanafalsafa wa China, Laozi alisema: “He who does not trust enough will not be trusted.”
Anamaanisha, imani inaanza na wewe. Waamini wenzako ili na wao waweze kukuamini. Usiwe mtu wa mashakamashaka. Kama una mashaka ni bora kutoingia kabisa kwenye uhusiano. Ishi na mtu unayemuamini.
source https://utamuzaidiapp.blogspot.com/2020/01/uaminifu-ni-muhimu-kuliko-mapenzi.html
No comments:
Post a Comment