Tuesday, January 28, 2020

NASAHA MUHIMU KWA WANANDOA NA WANAOTARAJIA KUINGIA KWENYE NDOA


Image may contain: 1 person
1. Amueni kupendana hata katika nyakati za changamoto. Upendo ni kushikamana na mwenzako, sio hisia tu.

2. Daima pokea simu ya mumeo/mkeo anapokupigia na ikiwezekana izime simu yako au ondoa mlio unapokuwa pamoja naye.

3. Upe kipaumbele muda wa kukaa naye. Fanya utaratibu wa kuwa na USIKU WA MUME/MKE kama tulivyofundisha kanisani. Muda ndio “sarafu ya ndoa” hivyo wekeza muda kwenye ndoa yako. Hakikisha uwekezaji wako unakuwa endelevu.

4. Shikamana na marafiki watakaoifanya ndoa yako iwe imara, achana na wale watakaokufanya uwe na MTAZAMO HASI.

5. Lifanye tabasamu na kicheko kuwa ala ya ndoa yenu. Furahini pamoja, na hata katika nyakati ngumu tafuteni sababu ya kufurahi na kucheka. Wale wanaocheka pamoja, hudumu pamoja.

6. Katika kila mabishano, kumbuka kuwa hakuna “mshindi” na “mshindwa”. Nyinyi ni washirika katika kila kitu, hivyo nyote mtakuwa washindi au nyote mtashindwa. Unganeni kutafuta suluhisho la tatizo.

7. Kumbuka kuwa ndoa imara ni nadra kuwa na watu wawili imara kwa wakati mmoja. Utakuta mume na mke wanapeana zamu ya kuwa imara pindi mmoja wao anapokuwa dhaifu.

8. Yape kipaumbele maisha ya kitandani. Ili kuwa na ndoa imara unahitaji zaidi ya tendo la ndoa, lakini ni vigumu kujenga ndoa imara bila tendo la ndoa.

9. Kumbuka kuwa ndoa sio 50-50, talaka ni 50-50. Ndoa inatakiwa kuwa 100-100. Ndoa sio kugawa kila kitu nusu kwa nusu, bali kila mmoja anatakiwa kila kitu kwa mwenzake.

10. Mpe mwenza wako kitu bora kabisa, sio mabaki baada ya kumpa kizuri mtu mwingine.

11. Jifunze kutoka kwa watu wengine, lakini usiyalinganishe maisha yako au ndoa yako na watu wengine. Kila mtu ana maisha yake ya kipekee kabisa.

12. Usiipe likizo ndoa yako wakati ukiwalea watoto wako, vinginevyo unaweza kutoka kapa.

13. Msifichane mambo ya msingi. Usiri ni adui wa mahabba ya kweli.

14. Msiongepeane. Urongo huvunja uaminifu na uaminifu ndio msingi wa ndoa imara.

15. Unapofanya kosa, kubali na uombe msamaha kwa njia nzuri. Unatakiwa kufanya haraka kusema: “Nilikosea. Kumradhi. Tafadhali nisamehe.”

16. Mumeo/mkeo anapokukosea, fanya haraka kumsamehe. Hilo litakupatia tiba ya moyo na kutengeneza fursa ya kujenga upya upendo wenu. Fanya haraka kusema: “Ninakupenda. Tusonge mbele.”

17. Vumilianeni. Mwenza wako daima ni muhimu zaidi kuliko ratiba zako.

18. Tengeza ndoa ambayo itawafanya watoto wako wa kiume wapende kuwa waume wazuri na mabinti zako wapende kuwa wake wazuri.

19. Unatakiwa kuwa mhamasishaji mkuu wa mwenza wako, badala ya kuwa mkosoaji wake mkuu. Unatakiwa kuwa mwenye kumfuta machozi badala ya kuwa mwenye kumsababishia machozi.

20. Kamwe usimzungumzie vibaya mwenza wako kwa watu wengine au kumtia kasoro au kumkosoa hadharani au mtandaoni. Mlinde mwenza wako nyakti zote na mahala popote.

21. Mnatakiwa kuswali wote. Kila ndoa huwa imara zaidi pindi mnapokuwa karibu na Mungu wenu.

22. Usifikirie talaka kama chaguo lako. Kumbuka kuwa “ndoa bora” hutengenezwa na watu wawili ambao sio wakamilifu na ambao hawako tayari kuachana.


source https://utamuzaidiapp.blogspot.com/2020/01/nasaha-muhimu-kwa-wanandoa-na_29.html

No comments:

Post a Comment