Tuesday, February 4, 2020

KATIKA MAPENZI HAKUNA CHA KUPUUZIA, KUWA MAKINI

Image result for KATIKA MAPENZI HAKUNA CHA KUPUUZIA, KUWA MAKINI




Mapenzi ni kitu cha tofauti kidogo. Umeshawahi kuona watu wakiwa ndani ya mapenzi moto moto? Umeshaona wanavyokuwa wakiwa pamoja? Hata kama wana miaka sitini ila wakati mwingine huwezi kutofautisha matendo yako na watoto.
   Hapo ndipo mapenzi yanapohitaji nafasi yake ili uweze kuyaelewa vizuri.
Mapenzi yanalugha ya ajabu sana. wakati unapoweza kumjibu rafiki yako “poa tu” na isilete matatizo ila katika mapenzi hapa kuna tatizo. Hapo mwenzako anaweza kuhisi umekasirika, anaweza kudhani sasa hivi humuheshimu kama zamani – ilmradi tu. Hapo ndipo mapenzi yanapohitaji nafasi zaidi. 
  Kila unachofanya kwa mpenzi wako  kina maana kubwa hata kama hujadhamiria. Unapopokea simu haraka anapokupigia inaleta maana f’lani kwake hata unapochelewa pia anapata maana. Tofauti ni moja tu, pale atapata maana nzuri kuwa unamjali na kumuheshimu wakati huku atapata maana  hasi- inayoweza kumpa wasi wasi na wahka katika nafsi yake. Katika mapenzi hakuna kitu kidogo!
   Simu yako kwake ina maana, sms yako ina maana hata aina ya utani unaomletea pia unamletea tafsiri f’lani katika akili yake. Kuna utani mwingine ukimfanyia anajiuliza mmmh… ni utani huu? Au kafikisha ujumbe kwa namna tofauti? Hayo ndiyo mapenzi. Ambayo yanamfanya mpenzi wako akuombe salio na ukimtumia yote anatumia kuongea na wewe, tena ukiangalia kwa haraka unaweza kusema hakuna neno la maana alilokwambia.
  Ila jua kitendo cha kukupigia simu tu kwake na kwako pia kina maana. Kwake kukupigia simu ni faraja kubwa kwa sababu kaongea na mtu anayemuamini na kumkabidhi hisia zake. Mtu ambaye ana mamlaka ya kumuuliza jana kwanini ulichelewa kulala ama kwanini leo umevaa hivi. Mtu wa kipekee aliyeamua kumruhusu kuwa na neno juu ya maisha yake. Hayo ndiyo mapenzi!
    Anakupigia mara kwa mara si kwa sababu hana watu wengine wa kuongea nao –  hapana. Ni kwa kuwa anakujali na kukuthamini. Ukiona suala hilo ni dogo basi mwenzako ataona humthamini wala kumjali. Ataona unamdharu. Ataona anajipendekeza kwako.
   Unajua matokeo ya fikra za namna hiyo zikimea katika kichwa chake? Ni kujiona hayuko na mtu sahihi katika maisha.
    Thamini kila unachofanyiwa na mwenzako bila kuangalia ukubwa wala thamani yake. Katika mapenzi kila jambo lina nafasi yake ya kuyajenga ama kuyabomoa mahusiano yenu. Ukiona kumpigia sana simu ni usumbufu, we acha tu. Ukiona kumwita majina ya kimapenzi mwenzako si kitu, sawa tu. Ila unapaswa kukaa tayari kwa matokeo ya bomu unalotengeneza. Ukae vizuri pale mwenzako atakapokwambia ama kuwaeleza marafiki zake humjali wala humthamini.
   Vijengavyo mapenzi ya kweli si magari na kupelekana ‘out’ Dubai tu ila ni kila jambo la kimapenzi ulifanyalo kwa mwenzi wako bila kujali ukubwa wala thamani yake.
    Thamani ya tendo unalomfanyia mwenzako litaamuliwa na kiwango cha hisia alicho nacho juu yako nafsini kwake. Kama mtu hana hisia na wewe hata umfanyie nini atafurahi na kukuona wa kawaida tu ama mwenye pesa sana. suala ni hisia. Mapenzi ni hisia.
    Na mwenye hisia na wewe kila jambo kwake ni muhimu. kauli ndogo tu zimeweza kurejesha amani na upendo katika nyumba nyingi, pia kauli zingine ambazo pia ni ndogo zimesababisha nyumba nyingi kuvunjika. Kuwa makini na matendo na kauli zako kwa mwenzako. Hakuna kidogo katika mapenzi. Kila jambo lina thamani yake.


source https://utamuzaidiapp.blogspot.com/2020/02/katika-mapenzi-hakuna-cha-kupuuzia-kuwa.html

No comments:

Post a Comment