Tuesday, February 4, 2020

Zijue tabia 10 hatari katika mapenzi



MADA yetu ya unyumba ni nguzo ya mapenzi, ukiwa mchoyo unabomoa, niliifafanua kwa matoleo mawili mfululizo. Bila shaka, utakuwa umetambua jambo la kuzingatia ili uishi kwa amani. Nyongeza ni kuwa kama binadamu na uhusiano wa kimapenzi, heshima ya kweli ni pale ambapo mwenzi wako anakutunzia ‘tamu’ yako kwenye mazingira yoyote yale.Akiitoa, ni sawa na kuvuliwa nguo! Pale unapopumzika na wengine hutulia hapo hapo! Hii inamaana kuwa hutakiwi kujiuguza uvivu katika suala la mapenzi. Toa huduma inayotakiwa, ikibidi ongeza vionjo kadiri unavyoweza. Kosa kubwa kwa wengi ni kwamba hawachukulii tendo kama ni jukumu la kutekeleza. Yaani ni wajibu! Wanaona ni kitu rahisi ndiyo maana kila siku wanalia.Unaacha kutekeleza nguzo hiyo ya uhusiano, matokeo yake mwenzi wako kwa kuzidiwa anaona bora aende akapate tulizo nje. Angalia unavyoweza kubomoa uhusiano wako. Anapoonja pembeni, kisaikolojia na hisia zake akizipeleka huko ni hatari zaidi, kwani anaweza kukuona huna faida.Ipo mifano mingi ya watu waliosahau nyumba zao kwa sababu ya manjonjo ya nje. Mume kumuona mke wake ni kapi, vivyo hivyo, mke kumshusha thamani mwenzi wake. Hayo yote yanaweza kudhibitiwa ikiwa kutakuwa na maridhiano ya kweli baina ya wanandoa. Anahitaji, jihimu kumtekelezea kwa maana hujui ndani yake kuna nini.Somo lilikuwa poa sana lakini tuachane nalo na kushika hili la leo. Tunazungumzia mapenzi katika sura ya kipekee kwa kuwa yanahitaji thamani ya hali ya juu. Yanaheshimiwa kupita kiasi kwa sababu yenyewe ni sanaa kiranja ambayo kila mtu lazima atayapitia.Tunapenda na kupendwa, hivyo tupo mapenzini. Ambaye hayumo, basi pengine mambo yake siyo mazuri. Hata hivyo, binadamu hatuko sawa, kila mtu anayo tafsiri yake anayoijua kuhusiana na mapenzi, ndiyo maana hatuachi kuelekezana. Naandika kwa kushauri na kukosoa kwa sababu huu ndiyo wajibu wangu katika safu hii.Kila mmoja anapoingia katika uhusiano wa kimapenzi, moja kwa moja ndoto zake huwa ni kumfanya mwenzi wake kuwa wa kudumu. Atajiwekea malengo hata yasiyotekelezeka ilimradi airidhishe nafsi yake.Hujawahi kuona mtu anapata mwenzi leo, kisha akaanza kupiga mahesabu ya kufunga naye ndoa? Ukweli ni kwamba wengi wetu tunapopata penzi jipya, tunakuwa na matarajio mengi. Ni vizuri kuwa na matarajio na kujiwekea malengo ya kuyatimiza, lakini kosa kubwa ni kwamba huwa tunajisahau katikati ya safari.Tunapenda kudumu na wenzi wetu tunaowapata, lakini ndoto hizo hugeuka za alinacha kama si kitendawili kwa kuwa hatuwezi kujirekebisha au kuficha makucha. Matunda ya hali hiyo ni kuwa na kizazi chenye kujiwekea matarajio ya ‘blah blah’ kila siku.Pointi ya msingi hapa kama kweli tunataka kuwa na mapenzi ya kudumu ni kujua udhaifu wetu angali bado mapema. Kutambua mambo ambayo ni sumu zinazoweza kuua uhusiano wetu ili tuzichukue kama changamoto, kisha tuzikabili na kushinda.Hapa chini, nimekuandalia tabia 10 ambazo ni sumu katika mapenzi. Hizi, zinaweza kuubomoa uhusiano wako ndani ya muda mfupi. Muhimu ni kuzijua ili utambue namna ya kuziepuka.Unaweza kuziepuka kwa sababu siyo za maumbile, bali ni kujiendekeza. Ukiamini hakuna kitakachoshindikana, kwa hiyo nakuasa uongozane na mimi mdogo mdogo ili upate jawabu la kutosha kuhusiana na mada hii.UVIVU
Hii ni sumu kali, lakini ni rahisi kuiepuka kama utaamua. Asili ya umbile la kila binadamu, ndani yake kuna uvivu. Ni vizuri kutambua kuwa katika vitu ambavyo ni rahisi kumchefua mwenzi wako ni hili la uvivu.Uvivu unaweza kuwa wa kujishughulisha katika mambo ya nyumbani ama wa utafutaji wa riziki. Lakini baki ukijua kwamba tabia hiyo inakufanya ukalie kuti kavu kwenye uhusiano wako.Unashindwa kumsaidia mpenzi wako kazi ndogo ndogo, unangaalia nguo chafu haujitumi kuzifua, nyumba haitamaniki, hujiwezi kwa lolote, tabia yako hiyo, inampa mwenzio tiketi ya kukuacha.
Pointi hii, inastahili kupigiwa mstari mwekundu kwetu sisi wanawake.Ni rahisi mwanaume kuvumilia kasoro chache alizonazo mwenzake, lakini siyo ya namna hii. Muhimu ni kutambua ya kwamba uvivu utakupunguzia heshima na mvuto wako katika mapenzi.Aidha, kwa mwanamke ni janga ambalo mwanaume hatokawia kulikimbia. Unadhani atawezaje kuvumilia kuwa na mtu ambaye hajiwezi kwa lolote? Kujishughulisha hutaki, kuwajibika katika uwanja wa kuta nne ni ngoma nzito! Atajiuliza: Ni faida gani ya kuwa na wewe?UCHAFU
Tabia hii, inaenda sambamba na uvivu. Kwa kifupi ni kwamba uchafu ni matokeo ya uvivu. Mtu asiyejiweza kwa lolote hatomudu usafi, hivyo kutia sumu kwenye uhusiano wake.Una tabia ya uvivu, kwahiyo ni mchafu, unapaswa kutambua kuwa mwenzi wako anakerwa mno na tabia yako. Anza kwa kujichunguza mwenyewe ili kujua wewe ni mchafu kwa kiwango gani. Jawabu lako, linaweza kukusaidia kwa kiasi cha kutosha, ikiwa utaamua kubadilika.Unavaa nguo mpaka zinatoa harufu mbaya, ukiongea, unatoa hewa chafu ya mdomo, kuoga kwa wasiwasi hadi mwili unanata, unashindwa kudhibiti jasho lako, mpaka unawasumbua wenzako kwa sababu ya kikwapa, kwa hali hiyo unategemea nini?Tuweke kituo kikubwa kwa leo, panapo majaliwa tukutane Jumatatu, tupate kuendelea na mada yetu hii. Ushirikiano wako bado nauhitaji, kwahiyo tumia namba yangu hapo juu kwa ushauri au maoni.Kama utakumbuka vizuri shoga yangu, katika toleo lililopita la Ijumaa Wikienda, niliweza kuchambua sumu mbili kati ya 10 zinazounda mada hii. Sina shaka kwamba ulinisoma vya kutosha, hivyo nakuomba uungane nami tena leo ili tuendelee pale tulipoishia.Nilieleza Uvivu na Uchafu kama sumu zinazoshabihiana, kwahiyo zimebaki nane. Kabla sijaendelea mbele, naona ni busara nikuulize swali moja; Umejifunza nini mpaka sasa, kutokana na mada hii? Jibu naomba unitumie kupitia namba ya simu iliyopo hapo juu.UBISHI
Unyenyekevu ni mbolea ya mapenzi, kinyume chake ni sumu, ndiyo maana ubishi ukawa tindikali ya uhusiano. Changamoto hii, kama ingekuwa inaeleweka vizuri na kuzingatiwa inavyotakiwa, pengine kusingekuwa na watu wanaotengana.Binadamu tumeumbwa na udhaifu, kwahiyo kukosea siyo vibaya kwakuwa ni sehemu ya maisha yetu. Pamoja na kulifahamu hilo, lakini wengi wetu huwa hatutaki kukubali ukweli katika yale tunayokuwa tumekosea.Tunataka tushinde kwa hoja hata kwenye mambo ambayo tunastahili kuwaomba radhi wapenzi wetu. Kasumba ya namna hiyo huwaumiza wenzetu moyoni kwa sababu wao huamini wamekosewa, kwahiyo hutarajia angalau kuombwa msamaha.Fikiria mpenzi wako amekufanyia kosa ambalo wewe unalitathmini kama ni kubwa, unamuweka chini unaongea naye, lakini mwenzako anakuruka futi hamsini. Hataki kukubali kosa na zaidi anataka mbishane mpaka majogoo yawike. Katika picha ya namna hiyo wewe utajisikiaje?Maumivu utakayoyapata wewe, basi yaone kuwa ndiyo anayopata mwenzako kutokana na tabia yako ya kutotaka kukubali ukweli. Mkuki kwa nguruwe kwa binadamu mchungu, msemo huu una maana kubwa kwa sababu tunapenda kuwaona wengine wabishi, lakini yakiwa kwetu hatutaki kujikosoa.KIBURI
Kama ilivyo uchafu unatokana na uvivu, ndivyo ilivyo kwa Ubishi unavyoleta Kiburi. Maana yake ni kwamba mtu unapokuwa mbishi kupitiliza, unavimba kichwa na huko ndiko kuelekea kwenye kiburi. Utaelezwa nini na wewe kila kitu unajua?Asili ya mtu mwenye kiburi huwa na majivuno kwa kuamini kwamba hakuna kinachoweza kumbabaisha. Lakini mtu mwenye fikra hizi anakuwa amepigwa kikumbo na tafsiri ya mapenzi ambayo inasema ni mwiko kujifanya ‘much know’ mbele ya mwenzi wako.Daima kila unaloelekezwa hufanyi, badala yake unakuwa mzuri katika kupuuzia mambo. Ukichekecha kichwa chako, utagundua kwamba upuuzi ni sehemu ya kiburi, mnapanga miadi wewe na sweetie wako mkutane mahali, lakini unaamua kutokwenda bila sababu ya msingi.Mpo katika maongezi ya faragha, mwenzio anajaribu kukuelewesha katika maeneo ambayo huwa unakosea, lakini badala ya kupokea ukweli, unaamua kunyamaza kimya, halafu unamkunjia sura kana kwamba anachokwambia ni simulizi za kubuni. Hicho ni kiburi!Ukweli upo hivi, mtu mwenye kiburi akiambiwa ukweli huamini ametukanwa, hivyo huzua visa vya uongo na ukweli ama kubisha bila hoja, ndiyo maana nilitangulia kusema kuwa kiburi ni zao la ubishi.Kasumba hii ukiwa nayo ni rahisi kuachwa kwa sababu hakuna siku ambayo mpenzi wako atakuwa anajisikia faraja kuwa na wewe.Atakuona mzigo kwa kuwa ataamini haumheshimu na ukichunguza inakuwa kweli, kwani ungekuwa unamtii, usingembishia ama kumvimbia kwa kiburi chako.NYODO
Najaribu kuzipanga pointi katika mtiririko unaofaa,  nikiamini kuwa ndiyo itakuwia rahisi kuelewa.  Aghalabu, mtu mwenye kiburi ndiye huyo huyo mwenye nyodo. Unakuwa bingwa wa mapozi na michetuo mbele ya mwenzi wako, lakini mapenzi hayataki hivyo!Hakuna kitu kibaya kama kujiona babkubwa katika mapenzi. Saikolojia inafundisha kwamba ukiwa memba katika uhusiano fulani, basi unatakiwa kuishi kulingana na jinsi ulivyo. Tafsiri ya sentensi hiyo ni kuwa unashauriwa kuishi rahisi, kutokana na jinsi alivyo mpenzi wako.Si busara ukiwa na mwenzi wako, halafu unakuwa unaongelea mambo makubwa ambayo haoti kuyaona sembuse kuyapata. Au unakuwa bingwa wa kubagua chakula, kwa kukiona ni cha gharama nafuu, huku ukiwa kiongozi wa kuomba misosi ya bei mbaya.Mpenzi wako anajitutumua kukununulia zawadi, badala ya kushukuru, mwenzetu unapokea huku ukibetua midomo kuonesha kwamba siyo za hadhi yako. Picha hiyo, ukimuonesha mara tatu, halafu akiendelea kukupa zawadi, pengine huyo mwenzako atakuwa na matatizo kichwani.Anapanga vizuri mambo yake, anakuomba mtoke wote, mnafika kiwanja, unaanza kukishusha thamani, halafu unakosa raha kabisa kuwepo eneo husika. Taswira kama hiyo unapomuonesha mwenzako, itamvunja moyo na atajuta kutoka na wewe.Muhimu hapa ni kuridhika na kile unachopewa, hivyo ndivyo mapenzi yanataka. Anachokupa shukuru kwa kuwa ndicho alichojaliwa, siku akipata zaidi atakupa cha thamani kubwa. Kinyume chake ni kumkera kwa kuwa atakuona una nyodo na haufai kuwa mpenzi wa kudumu.DHARAU
Hapo juu nimeshaeleza kuwa NYODO inatokana na KIBURI kwa sababu mtu mwenye nyodo na kiburi ni kama shati na fulana au viatu na soksi.Sura hiyo ndiyo iliyopo katika DHARAU na NYODO. Ni kama shamba na bustani, nikimaanisha kwamba tabia hizi zinatafsiri zenye kukaribiana lakini nazitofautisha katika mada hii ili kila moja ibebe uzito wake.Dharau ni sumu kubwa katika uhusiano wowote. Ukiwa na sifa hii, unatakiwa kujishtukia kuwa wewe ni vigumu kukubalika mbele ya mtu mwingine yeyote na zaidi ni katika mapenzi, kwani hakuna atakayeweza kukuvumilia.Kikubwa hapa ni kujua kuwa mara unapokuwa katika uhusiano na mtu fulani, basi yule ni mwenzako. Shirikiana naye katika hali zote. Kama ana upungufu, jukumu lako ni kuubaini mapema na kujitahidi kuurekebisha. Kumzodoa ni alama ya dharau.Marekebisho yawe ni katika kila unaloona halikupendezi kutoka kwake. Yawezekana mavazi yake yakawa yanakupa kichefuchefu, kwa hiyo unapaswa kulivalia njuga suala hilo ili umuweke mpenzi wako kwenye sura ambayo inakuvutia.Kumshusha thamani ni dharau na ukimuonesha akaelewa unamdharau, hiyo ni sumu kali katika uhusiano wako. Ni vizuri kutambua kwamba mapenzi ni sanaa inayojengwa kwa hisia, kwa hiyo kudumu au kutodumu kwa penzi lako, kutategemea na unavyocheza na hisia za mwenzako.Hupendi staili yake ya maisha, hilo ni jukumu lako. Maisha ya nyumbani kwao ni ya shida, elewa hali hiyo ni matokeo na kwamba kupata ni majaliwa. Anaumwa yeye mwenyewe, mzazi au ndugu yake yeyote, ni vizuri kutambua kuwa kabla hujafa hujaumbika.Ukijua hayo, basi hutamtoa kasoro mwenzako na badala yake utashiriki kumsadia pale unapoweza. Ukifanya kinyume chake ni ishara nyingine ya dharau na akijua unamuona wa bei chee ataona unamnyanyapaa.UONGO
Tafsiri yake ni tabia ya kutosema ukweli, yaani ujanja mwingi na kudanganya ili kujiweka katika mazingira salama. Pamoja na ukweli kwamba wengi huutumia katika kujipa ushindi wa mezani, lakini hii ni sumu nyingine kali kwenye uhusiano wa kimapenzi.Maana nzuri katika tafsiri fupi ni kuwa uongo ni dharau kwa kuwa ungemheshimu, usingemdanganya. Mtu anayemuongopea mpenzi wake, huyo si muoga kwenye uhusiano, hivyo anakuwa amepitwa na nguzo muhimu ya kulifanya penzi lake lidumu kwa miaka mingi.Ukichunguza kwa makini, asilimia kubwa ya watu waliodumu na wenzi wao ni wale wanaoishi kwa hofu katika uhusiano. Anauheshimu, kwa hiyo anaogopa kuuvunja. Anaweka mikakati ya kujiweka salama mbele ya laazizi wake. Lakini hayo si ndiyo mapenzi?Aidha, ukichunguza tena kwa makini, utabaini kuwa uongo, maana yake ni kujiona unajua vitu vingi kuliko wengine. Wewe ni fundi wa kugeuza maneno na unaweza kumfanya mtu aamini moja jumlisha moja ni tatu. Mapenzi hayataki hivyo!

Share this:


source https://utamuzaidiapp.blogspot.com/2020/02/zijue-tabia-10-hatari-katika-mapenzi.html

No comments:

Post a Comment