Saturday, February 1, 2020

KAMA UNGEJUA MKEO ATAKUWA NA TABIA ALIYO NAYO SASA, UNGEKUBALI KUMUOA❓

 (a) Ningekubali (b) Nisingekubali
✍️ Katika swali hili, wanaume 79 walisema wasingekubali! Wanaume 12 walisema wangekubali. Ungetegemea kuwa akina Mama ndio wanaoishi maisha magumu katika Ndoa, lakini kwa majibu haya ni dhahiri kuwa akina Baba wengi nao wana machungu makubwa ndani ya Ndoa zao. Katika majibu yake, Mwanaume mmoja alisema kuwa, anajuta kuoa Mwanamke aliye naye kwa sababu amekuwa na maisha magumu sana tangu wawe pamoja. Mkewe amesababisha akorofishane na ndugu zake wote. “Hataki kabisa kuona ndugu zangu wakija nyumbani kwangu wakiwemo Wazazi wangu. Wanapofika huanzisha vurugu na ugomvi wa makusudi na hufikia kiwango cha kuwasimanga na kuwatukana Wazazi wangu bila aibu”
✍️Wanaume waliochoka Ndoa zao wamesema kuwa Wake zao sio waaminifu kwa vile wamegundua wana Wanaume wengine nje ya Ndoa na wengine wanaendekeza ushirikina kwa nia ya kuwafanya Waume zao watulie nyumbani.
✍️Mmoja anasema kama isingekuwa maombi ya waamini wenzake, angeshapoteza maisha. “Mke wangu aliniwekea dawa kwenye chakula ili niwe namtii kila asemacho. Dawa hii nasikia alipewa na mganga mmoja huko Bagamoyo. Matokeo ya dawa ile ilinifanya nipooze upande mmoja wa mwili wangu na niliteseka sana na maradhi hayo hadi pale watu wa kanisani kwangu walipokuja kuniombea na kisha kunipeleka katika mikutano ya Kanisa hadi nilipopona”
✍️Wengine wamelalamikia tabia ya dharau, matusi na umbea zinazofanywa na Wake zao. “Nimekwisha hama zaidi ya nyumba sita hapa mjini kwa ajili ya tabia za umbeya wa Mke wangu. Kila wiki vikao vya kusutwa na kupigwa faini. Yaani ni aibu juu ya aibu” wakati huyu anasema hivi, mwingine alieleza kwamba, Mke wake hatulii na anabadilisha Wanaume kama nguo. “Kibaya sana anaweza kutembea hata na marafiki zangu. Ameshafumaniwa mara mbili nikalazimika kuomba uhamisho toka Iringa kuja hapa ili kuepuka aibu, lakini hata huku mambo yamekuwa yale yale’
Ninaishi kwa amani na mke wangu ama kwa hakika nimemchoka na hata natamani kuoa mke mwingine
JE, UMEOA/KUOLEWA NA MTU ULIYEMTAKA; NI CHAGUO LAKO HALISI
(a) Ndiyo (b) Hapana
Katika majibu ya swali hili, wengi wamekiri kufunga ndoa na watu ambao kwa kweli hawakuwapenda kwa dhati na hawakuwa chaguo lao. Katika kundi hili, Wanawake wanaonekana kuathirika zaidi. Wanaume 49 walisema walifunga ndoa na Wanawake ambao hawakupanga kuwaoa. Nao wanawake 73 walisema waliolewa na Wanaume ambao hawakuwa chaguo lao. Kwa lugha nyingine, ndoa 122 kati ya 200 zilifungwa pasipo hiyari wala upendo wa dhati wa Wanandoa wenyewe. Je, hali hii imetokana na nini
Zipo sababu nyingi zilizosababisha hali hii kama wahusika wenyewe walivyojibu katika maswali haya. Ingefaa tuziangalie kwa uchache tu zile zilizobeba uzito mkubwa zaidi.
Mwanamke mmoja anasema hivi katika jibu lake;- “Huyu hakuwa Mchumba wangu, ila nilikuwa naye kama rafiki wa kutoka naye mara moja moja. Bahati mbaya wambeya walimpelekea taarifa Mchumba wangu ambaye aliweka mtego na siku moja akaninasa. Sikuwa na jinsi zaidi ya kumlazimisha huyu anioe ingawa ilichukua muda mrefu kukubali. Kwa kweli ni mimi ndiye ninayeonesha kumpenda wakati yeye, wala hajali kitu chochote kwangu"
✍️Jibu lake liliungwa mkono na Wanandoa wengi. Hii inaonesha kuwa udanganyifu na ukosefu wa uaminifu wakati wa uchumba ni mkubwa. Wachumba wengi wanaendeleza tabia ya kuwa na marafiki wengine wanaoshirikiana nao hata kufanya ngono.
✍️ “Unajua kwa sisi Wanawake huwezi kuamini kuwa huyu uliye naye atakuoa kweli kwa sababu wengi wanakwambia wanakupenda lakini baada ya muda wanakuacha. Kwa jinsi hiyo, unalazimika kuwa na mtu mwingine wa akiba ili huyu wa sasa akikutupa upate pa kukimbilia”. Maneno haya ya kujitetea yanatia simanzi na kuonesha kuwa chanzo ni kikubwa cha matatizo yanayozuka hata baada ya Ndoa.
✍️Wanaume waliojibu swali hili, walisema walilazimika kufunga Ndoa na Wake zao baada ya kuwapa ujauzito. “Sikupanga kuwa na Mke huyu. Nilimwoa baada ya kulazimishwa na Wazazi hasa pale alipopata ujauzito na Wazazi wake wakatishia kunipeleka mahakamani kama nisingemwoa. Kwa kuwa niliogopa kuipa familia yangu na mimi mwenyewe fedheha, niliamua kumuoa” anasema Mwanandoa mmoja. Sababu hii ilitolewa pia na Wanawake ambao walisema hawakuwa na namna ya kukwepa kuolewa na Wanaume wa sasa baada ya kupata mimba “isiyotarajiwa” na hivyo kukubali kuolewa.”Mimi nilikataliwa na mchumba wangu niliyempenda sana baada ya kugundua kuwa nimepata ujauzito wa mtu mwingine. Yeye kwa sasa ameoa, lakini kwa kweli nilimpenda Mwanaume yule na bado nampenda hata sasa” anakiri Mama mmoja katika majibu yake. Ni wazi kuwa wengi wetu tumefunga Ndoa katika namna ambayo hatukuwa tumepanga.
✍️Baadhi ya Wanandoa walisema kuwa, walilazimika kuoana kwa sababu ya shinikizo la Wazazi. Mmoja alisema alimwoa Mkewe baada ya Wazazi wake kumkataa mchumba aliyemchagua kwa vile hawakutaka kuletewa Mwanamke asiye wa kabila lao. “Nami kwa sababu sikutaka kuwakorofisha Wazazi wangu, na kwa vile pia jamii yetu inaheshimu sana Wazee na kama njia ya kukwepa laana, niliwakubalia wanipe huyu Mke niliye naye.
Ni kweli kwamba Wazazi wanao wajibu wa kuhakikisha kuwa watoto wao wanapata wenzi wema. Kitabu cha Hekima ya Yoshua Bin Sira kinaeleza wajibu wa Wazazi kuwapatia vijana wao wenzi wao wa ndoa..‘ikiwa una Watoto uwarudi, bali uwapatie Wake zao wakati wa ujana wao. Umwoze binti yako, nawe utakuwa umemaliza jambo kubwa; tena umpe mtu mwenye ufahamu’ (YBS. 7:23,25)
✍️Pamoja na haki hii ya Wazazi, ingelikuwa busara sana jambo hili likafanyika kwa umakini na busara na kuwapa Watoto wao haki na ruksa ya kuchagua Mke ama Mume anayemwona ni mwema kwake, hata kama Wazazi wanaona kuwa huyo ni masikini ama hataweza kuwasaidia kwa kipato. “Usijinyime Mke aliye mwema mwenye akili, kwa maana neema yake hupita dhahabu (YBS. 7:19)
✍️Wazazi wengi huenda waliangalia mambo yasiyokuwa na tija. Matokeo yake hayakuwa kama walivyotegemea. Binti yao hakai kwa amani, kila siku masimango na manyanyaso kutoka kwa Mume. Anaishi kwa mateso na sononeko la moyo. Badala ya kuwapenda Wazazi wake, anawachukia kwa sababu wamemwingiza katika janga.
✍️Hata anapolazimika kufikisha kilio chake kwa Wazazi, hakuna linalofanyika kwa sababu Wazazi hawana “jeuri’ ya kumsema Mkwe wao kwa lolote. Mali walizopewa zimewafumba mdomo; hawana kauli tena. Ni kama walimuuza binti yao na sasa ni uamuzi wa mnunuzi kuamua atumieje bidhaa aliyonunua.
✍️Kumbe Wazazi walitakiwa kuwapatia Watoto wao wenza wenye sifa za wema, akili na neema na sio fedha, mali ama umaarufu.
✍️Utafiti umeonesha kuwa Wanandoa walioshindwa kuoana kwa sababu zilizo nje ya uwezo wao, bado wanaendelea na uhusiano wa kingono na hawajisikii kosa lolote kufanya hivyo. Wanaishi na wenzao wa Ndoa kama kinga ama hifadhi tu, lakini akili na mioyo yao iko kwa wale waliowapenda. Katika uhusiano kama huo, watu hawa huweza kufanya mambo ya aibu kubwa bila woga wowote.
✍️Mwanandoa mmoja alikiri kufanya ngono na Mwanaume aliyempenda kwa dhati na katika kudhihirisha upendo huo, ameshika mimba ya bwana huyo wa nje na hajali kama Mumewe wa ndoa atajua. “Siogopi kitu na hilo libwana lenyewe (hapa akimaanisha Mumewe wa ndoa!), likijua ndio itakuwa nafuu yangu maana atanifukuza na nitakuwa nimepata uhuru wa kwenda kuishi na kipenzi changu” anasema Mwanamke huyo.
✍️Mwingine alisema kuwa anafanya kila awezalo kuhakikisha kuwa anavunja Ndoa yake na ya yule Mwanaume ampendaye, ili waje kuishi pamoja. Katika hali kama hii, kuishi na Mwanandoa asiyekuwa chaguo lako, ni sawa na kuishi jela. Kama sio kwa sala na msaada wa Mungu, ndoa ya aina hii imekufa na daima haiishi ugomvi na visirani vya kila namna.
Mwanaume mmoja, anakiri kuoa Mke anayejua kuwa hampendi.
✍️Alifanikiwa kumwoa Mkewe baada ya kuwashawishi Wazazi wa binti kwa kutumia uwezo wake wa kipesa. Lakini pamoja na kumfanyia kila aina ya jema, kumnunulia hadi gari, lakini Mkewe hana mapenzi kwake. “Ni kweli Mke wangu hanipendi, ingawa namfanyia kila jema. Nimejaribu kumwonya hadi kwenda kwa Wazazi wake, lakini amesema wazi kuwa anayempenda ni Mwanaume mwingine” kadhalika, Mwanaume huyu anasema kuwa alijaribu kumtafuta huyo Mwanaume anayemzuzua Mkewe, lakini wazee walimshauri aachane na jambo hilo baada ya kujua kuwa alioa mahali asipopendwa akidhani kuwa fedha yaweza kununua upendo.
❤️Ndoa na IHESHIMIWE NA WATU WOTE 🙏 NA MALAZI YAWE SAFI 🙏 MAANA WAASHERATI NA WAZINZI MUNGU ATAWAHUKUMIA adhabu (Waebrania 13:4)


source https://utamuzaidiapp.blogspot.com/2020/02/kama-ungejua-mkeo-atakuwa-na-tabia.html

No comments:

Post a Comment