Saturday, March 28, 2020

MAMBO YA KUZINGATIA ILI KUWA NA MAHUSIANO YENYE MALENGO.


Jambo kubwa la kuzingatia unapoanzisha mahusiano ni kuhakikisha unajua kama uko ndani ya mahusiano yenye malengo, au ya kupita tu.
Lengo kuu ni kuwa ndani ya mahusiano yenye malengo kuwa baada ya muda fulani tutafunga ndoa na kuwa mke na mume milele.
Lakini hilo lengo halitatimia endapo hautakuwa makini na mambo yafuatayo:
1. UPENDO:
Je unampenda? Na unahakika anakupenda pia? Sio upendo wa mdomoni tu, vitendo pia vinaashiria upendo kati yenu.
Pia tazama chemistry yenu, kuna maelewano masikilizano kati yenu? Nakadhalika.
2 UTAYARI:
Kumpenda mtu ni hatua nyingine, na kuwa na utayari wa kuwa nae pia ni hatua nyingine.
Unapompenda mtu basi ni vyema kuhakikisha kuwa una utayari ndani yako wa kuupokea upendo wake, kujitoa kwake kihali na mali, kumjali, kumuheshimu, kumtunza, na kumthamini, kuwa tayari kuyapokea mazuri, madhaifu na mapungufu yake, kumuonyesha maana halisi ya upendo, na hata kuwa tayari kuwa anafaa kuwa mume/mke wako kwa hapo baadae.
Inshort, hii inaitwa kuandaa mazingira ya kuulea upendo wako kwake.
3. UCHUMI:
Mapenzi sio pesa, lakini pesa ni muhimu kwenye mapenzi ili kunogesha upendo.
Ni vyema kujua kama wewe uko vizuri kiuchumi ili kuepuka kuwa tegemezi, kama hauko vizuri, je unajituma kusaka maendeleo?
Na ujue kama mwenzako yuko vizuri kiuchumi na kama hayuko vizuri kiuchumi, basi je ana mikakati, malengo ya kufanikiwa kiuchumi, anajituma kujenga uchumi? Maana sio hana hela, halafu bado ni kula kulala, kazi hataki.
Asikwambie mtu, kuwa na uchumi mzuri ni jambo la muhimu, na kuwa na mtu mtafutaji na anajituma ni jambo zuri sana.
4. AKILI:
Hapa ndio kasheshe ilipo, Bora ukosee kujenga, kuliko ukakosea kuchagua mpenzi.
Akili inayozungumziwa hapa sio zile "PHD, Bachelor, Masters za vyuoni" No, maana kuna watu wana degree lakini akili zao ni sawa na wa chekechea.
Jambo la kutazama ni matumizi yake ya ubongo, maarifa aliyonayo, misimamo aliyonayo kwenye kila jambo, maamuzi yake ya busara, hekima aliyojaaliwa.
5. TABIA:
Hapa ndipo roho ya mahusiano ilipo. Tabia ndiyo inaweza fanya mkadumu, au mkaachana mapema.
Jiulize kabisa, tabia zake zinakuvutia? Mienendo yake je? Maadili yake? Na je yeye anavutiwa na tabia zako? Kama huwa analalamika hapendi tabia yako hii na hii, je upo tayari kubadilika kwaajili yake?
Na zile tabia ambazo wewe huzipendi kwake, yupo tayari kubadilika?
6. DINI:
Huu ndio mzizi pekee wa mahusiano yenye malengo ya ndoa.
Lazima utambue vitu viwili:
A: Imani yake:
Je dini yake na yako zinafanana? Kama sio sawa, je upo tayari kutoka kwenye yako na kwenda kwenye yake? Au yeye yupo tayari kutoka kwenye yake na kuja ya kwako?
Misimamo yako na wazazi na ndugu zako ipoje kuhusu wewe kubadili dini.
Hii ni muhimu, lasivyo unaweza kaa miaka 4 ndani ya mahusiano, then kipindi mnapanga kuoana, ukastukia mipango ya ndoa inaharibika sababu ya utofauti wenu wa dini.
B: Hofu ya Mungu:
Kuwa na mtu ambaye ana hofu ya Mungu ni jambo la busara sana.
Mungu ndiye kinga ya ndoa, sasa utatakaje kuingia kwenye ndoa na mtu ambaye yeye hana wazo la kumuabudu Mungu? Hana hofu ya Mungu.?
7. UMRI:
Umri una maana kubwa sana kwenye mahusiano, umri unaweza kutafsiri kama mahusiano yenu yatatawaliwa na utoto mwingi, ubabe mwingi, au aina gani ya mahusiano.
Embu fikiria unaingia kwenye mahusiano, wewe mwanaume una age ya miaka 20, na mwanamke ana age ya miaka 40, ambao ni umri unaoendana na wa mama yako nani atakua na nguvu ndani?
Mwanamke una umri wa miaka 18, unaolewa na mwanaume mwenye umri wa miaka 60, umri sawa na babu yako malengo ya watoto wenu itakuaje?
Inaashiria kwamba utakuja kuwa single mother kwa muda mrefu, au kuendana na huo umri wa mumeo, basi utajikuta unakuja kuyabeba majukumu ya kuilea familia sababu mumeo nguvu za kufanya kazi zinaelekea tamati.
Ni vyema mkawa mmepishana kiasi, na hasa mwanaume awe ndiye mkubwa.
Na kama mwanamke atakua mkubwa basi iwe amempita mwanaume kwa miaka michache sana, na mwanaume awe na uwezo mkubwa wa kuongoza na kutawala.
Umri sio namba, umri ni muhimu sana, na ni vyema kuuzingatia.
Upweke, pesa, au kuchelewa kuoa/kuolewa kusikufanye ukafanya hili kosa.
8. MALENGO:
Ni vyema kujua unaingia kwenye mahusiano gani, na mtu wa aina gani?
Ana malengo na wewe? Ana malengo na maendeleo yenu? Ni vyema kuepuka mahusiano yasiyo na malengo na wewe, unakua mchepuko wa mtu, au unakua chombo cha starehe cha mtu, ATM ya mtu.
Hebu hakikisha unakua ndani ya mahusiano ambayo uliyenae anawish aje kuwa mume /mke wako, na wewe unatamani aje kuwa mume/mke wako.
Jambo baya sana unakaa na mtu miaka 6 kama boyfriend na girlfriend, kumbe hana malengo ya kukuoa/kuolewa nawe, mwisho unakuja stukia anatoa/anaolewa na mtu mwingine, kipindi hicho ulishapoteza muda sana kwake.
Nadhani mpaka hapa utakua umepata kitu, wewe ambaye upo kwenye mahusiano, au unaanzisha mahusiano.
Hivi vitu usipovitazama kwa jicho la tatu, basi vina madhara makubwa sana kwa hapo baadae.
Unaishi na mtu unadhani anakupenda, kumbe hakupendi.
Hana tabia zinazokupendeza "kila siku zinakukera".
Hana matumizi mazuri ya akili yake.
Unahustle nae mwisho kwenu wanagoma usibadili dini.
Anakupenda lakin hana utayari wa kukufanya ujihisi unapendwa uone upendo wake kwako.
Mnahustle pamoja lakini mwisho ndugu wanakataa ndoa "Huwezi olewa na mtu ana umri sawa na babu yako", au mnaingia kwenye ndoa mkiwa bado vitoto, kiasi kwamba ndoa yenu ni utoto mwingi, ugomvi kila siku mpaka kero kwa wasuluhishaji.
Unaolewa na mwanaume ambaye akili yake kama mtoto vile, hana uwezo wa kujiongoza yeye mpaka wewe, misimamo ya kijinga, hekima na busara hazipo "yeye kwake ubabe tu na ukurupukaji".
Mtihani ni pale unapokaa miaka mingi na mtu asiye na mpango wa kukuoa/kuolewa nae.
Unaingia kwenye mahusiano na mtu ambaye hana utayari wa kukujali, hakuheshimu, hakutunzi. Mwingine ana uchumi mzuri lakini hana utayari wa kukutunza, anakupenda lakini kila siku kauli zake ni kukusimanga kwa madhaifu yako, au anajua ana mapungufu fulani, basi ndo mada yake hiyo kila siku mpaka ukerekwe.
Kuwa Makini Malengo yako yako mikononi mwako.
Unalolipanga leo ndilo litakalo kupa matokeo kesho.


source https://utamuzaidiapp.blogspot.com/2020/03/mambo-ya-kuzingatia-ili-kuwa-na.html

No comments:

Post a Comment