Tuesday, May 26, 2020

SIMULIZI; MUME WANGU ALIVYONISALITI SIKU YA SEND-OFF YANGU NA X WAKE!

UTAMUZAIDIAPP

Ilikua ni siku ya Send Off yangu, niliamini kua hiyo ndiyo itakua siku yangu, siwezi kuisahau kwani nakumbuka ilikua ni siku ya Alhamisi, baada ya kuhangaika katika mahusiano kwa miaka 7 sasa na mimi nilikua naolewa. Nilipambana sana mpaka kumpata huyu mwanaume kwani tulipitia mengi, usaliti na vipigo vya kila mara nilishavizoea.

Niliamini sasa atakua amebadilika kama ambavyo kila siku amekua akiniambia lakini kurudi kulekule kunisaliti waziwazi. Lakini kama wanawake wengine kwakua nilikua natamani sana ndoa basi nilikua tayari kuvumilia kila kitu, sitaki mnihukumu lakini ukiwa na miaka 33 na umekua kwenye mahusiano na mwanaume mmoja kwa miaka saba.

Umeshamtambulisha kwenu na kwao wanakujua naamini unakua huna uchaguzi sana wa nini chakufanya. Mchana nikiwa saluni napambwa kwaajili ya Photoshoot na sherehe usiku, meseji za Whatsaapp ziliingia katika simu yangu. Mdogo wangu aliniletea simu yangu, ilikua ni namba ngeni kabisa, ziliingia mfululizo kama kumi hivi.

Nilizifungua zote zilikua ni picha, nilifungua moja moja nakujikuta nabubujikwa na machozi, zilikua ni picha za mchumba wangu akiwa na mwanamke mwingine, ndiyo si mwanamke tu ni X wake ambaye kila siku tulikua tunagombana kuhusu yeye. Walipiga kitandani, mwanzoni nilijipa moyo kuwa ni picha za zamani lakini ni kama alijua kua nitawaza hivyo.

Mwisho alituma na picha ya Hoteli moja pale Iringa, ndiyo Hoteli ambayo mchumba wangu na ndugu zake walishukia, tena tuliwatafutia sisi, niliishiwa nguvu, hata kabla ya kufanya chochote iliingia meseji ya maneno “Wewe olewa kwenda kufua Boxer zake sisi tunatumia pesa zake”. Hazikua picha za kuibia, mchumba wangu alipiga akiwa na furaha kabisa, katika mapozi tofautitofauti.

Watu pale saluni waliona Mood yangu kubadilika, “Eliza ni nini?” Waliniuliza, sikua na jibu, nilinyamaza, nikijua watataka kuona harakaharaka nilifuta kila kitu. “Hamna kitu ni Denis alikua ananiambia kanimiss.” Nililazimisha tabasamu lakini machozi yalianza kutoka, Dada yangu alihisi kitu, alibadilisha mada ghafla. “Yaani na wewe na hayo mapenzi yenu, hivi utaacha kulialia lini kila saa akikutumia meseji!”

Watu walicheka na kunitania, lakini yeye alijua kuwa kuna kitu. Nilijikaza na kupambwa mpaka mwisho, baada ya kutoka pale aliniuliza kama kuna tatizo, nilimuambia hapana, niko sawa kuna mambo tu nilikumbuka. Sikuumia tu kwasababu mchumba wangu hakubadilika, hapana hilo ni kama nililijua, wakati nakubali kuolewa nilijua ni Malaya, nilijua hatabadilika kirahisi lakini niliumia kwa kutokuniheshimu.

Ilikua ni siku yangu ya kuagwa na ndugu zangu, hakuheshimu hata kuwa mbali na X wake angalau kwa siku moja. Alimchukua kutoka Dar na kuja naye mpaka kwenye sherehe, wakalala katika Hoteli moja, tena ambayo tulikua tumewatafutia na kuwalipia sisi. Niliumia sana, nilitamani kusema siolewei tena ila niilijua nitajidhalilisha na hiyo inaweza kuwa ndiyo ndoa yangu ya mwisho, nilijipa moyo atabadilika na kuacha mambo kuendelea.

***
Nilivumilia mpaka sherehe ilipoisha, sikutaka kumuambia kitu kabla kwani ingawa tulishafikia hatua za mwisho nilijua kama ningeongea kitu angeweza kuniacha hata kabla ya kufunga ndoa. Alijua kuwa nampenda sana hivyo alimua kunifanyia vituko vyote ili tu kuniumiza. Tulipoingia kwenye ndoa ndiyo nilimuambia lakini hata hakujali “Kama umechoka si uondoke kwani nani kakulazimisha kuolewa!”

Alinijibu kwa hasira na kujifanya kama mimi ndiyo nilikua nimemkosea adabu, mara kwa mara alikua akinipiga akiniambia ni mwanamke wa namna gani ambaye namhojihoji kila siku! Alikua akiniambia kuwa nataka kumkalia kichwani na maneno mengine kibao. Lakini bado nilivumilia, nilimuomba Mungu kwa kusali na kufunga, hakuacha tabia zake, kila siku alikua analewa hanihudumii na akirudi anadai chakula.

Wakati wa harusi kuna kiwanja tulipewa na wazazi wake, ilikua kama zawadi, kama miezi mitatu hivi baada ya ndoa nilipata ujauzito. Alikuja na kuniambia kabadilika, aliniambia kua anataka kuwa Baba hivyo ni bora kubadilika kwani hataki mtoto wake kuteseka, kweli alibadilika, alianza kunijali na kunishirikisha katika mambo ya maendeleo. Aliniambia kua anataka tujenge katika kile kiwanja kwani hataki mtoto azaliwe katika nyumba ya kupanga.

Kweli nilimuelewa hasa pale alipotaka tubadilishe jina la kiwanja kutoka jina la Baba yake na kuwa majina yetu. Nilimkubalia na kuanza mchakato, tukiwa katikati ya mchakato, alinishauri tuchukue mkopo, aliniambia ana akiba kidogo kama milioni tano lakini zisingetosha ujenzi hivyo kwakua mimi ni mfanyakazi wa serikali na nina mshahara mzuri tu nichukue mkopo ili tuweze kujenga kwa harakaharaka.

Aliahidi kuhudumia familia, ingawa nilikua na mashara lakini sikua na namna, mambo yalikua yanaenda vizuri, alishaanza kuniamini na kwakua alikua na nia nzuri sikuona sababu ya kutokuchukua mkopo, sikutaka kuyaharibu mambo. Nilichukua mkopo, kwa mshahara wangu kipindi kile niliweza kuchukua Shilingi milioni kumi na nne na laki sita. Baada ya kuzichukua nilimkabidhi kwaajili ya ujenzi.

Sikua na wasiwasi kabisa isitoshe bado nilikua napata kama laki tatu na thelathini kwa mwezi, kiasi kilichokua kimebaki katika mshahara wangu baada ya mkopo. Sikuamini macho yangu, siku tu niliyomkabidhi ile pesa hakurudi nyumbani, simu zake zilikua hazipokelewi.. Nilichanganyikiwa kwa kweli, nilimsubiria kwa wiki nzima lakini hakurudi nyumbani, niliwapigia simu ndugu zake hawakua wakijua chochote.

Ilinibidi kwenda kazini kwao ambapo walishangaa kwani alishachukua likizo, hapo ndipo nilichanganyikiwa zaidi na kujua kua nimeibiwa. Mwezi mzima uliisha ndipo aliporudi na nilipomuuliza kuhusu pesa alikasirika na kuniambia kuwa kama nimechoka niondoke, yeye ndiyo mwanaume hawezi kupangiwa cha kufanya, alinipiga sana siku hiyo hakujali hata kama nina mimba yake.

Sikua na chakufanya zaidi ya kunyamaza tu, tabia zilezile ziliendelea, mimba ilikua inanisumbua lakini hakujali. Kwa bahati mbaya sasa kipindi kile ndiyo Bodi ya mikopo ilianza kudai wadaiwa sugu, mimi nilikua mmoja wao nilisahaulika tu hivyo mchakato ulipanza jina langu lilipelekwa na kuanza kukatwa, tena kipindi hicho ndiyo Bunge lilishapitisha suala la asilimia 15. Nilichanganyikiwa kwani ilimaanisha kuwa sasa nilikua napokea mshaara kama laki mbili kasoro.

Ukipigia mahesabu nyumba ya kupanga, tena nyumba nzima, sina akiba yoyote na mimba juu, mume haonekani hahudumii hata senti moja nilichanganyikiwa. Lakini maisha ilikua ni lazima yaendelee, nilipambana hivyo hivyo mpaka nilipofikisha miezi nane kama na nusu hivi ya ujauzito. Zilikua zimebaki kama wiki mbili kujifungua, nikijua kuwa sina mtu wa kunihudumia nilipanga kwenda nyumbani.

Mume wangu hakua nyumbani hivyo ililazimu kumpigia simu ili angalau arudi abaki na nyumba kwani najua kama ningebaki pale ningechanganyikiwa. Alikuja, si kunisikiliza bali kuniambia niende kwao, nilishangaa kwani ndugu zake kwanza Mama yake alishafariki na walilelewa na Bibi yao ambaye ni mzee sana, isingekua busara kwenda kwani yeye mwenyewe anahitaji kuhudumiwa.

Alikataa na kusema kikwao mwanamke hujifungulia kwao la sivyo nibaki palepale, nilichanganyikiwa zaidi tukabishana sana kisha akaanza kunipiga, alinipiga sana na kuondoka huku akiniambia kuwa kama nikienda kwao basi nisirudi kwake. Niliumia sana, siku mbili nilikua na maumivu ndani, nilimpigia simu Mama ambaye safari hii aliniambia nifunge nyumba na kurudi nyumbani.

Mama yangu alikua mpole sana na kila siku nilipokua nikimuelezea matatizo ya ndoa yangu aliniambia vumilia, maneno yake yalikua yaoleyale ya kila siku kuwa ndoa ni uvumilivu na wanaume wote ndivyo walivyo. Lakini baada ya kumuambia vile aliniambia kuwa hakuna kuvumilia tena ni bora kuondoka na kama ataniacha basi aniahce.

Nilijiandaa na kurudi nyumbani kwajaili ya kujifungua, nilikua nimechoka na sikujali tena kama mume wangu atakasirika au la. Nashukuru Mungu pamoja na matatizo yote nilijifungua salama, mume wangu nilimpa taarifa za kujifungua lakini hakujali, hakuniambia hata hongera. Alijifanya kukasirika akiniambia kuwa simjali na sijali ndoa yangu. Kwa furaha niliyokua nayo sikujali sana kama anafuraha yeye au la.

***
Nilimaliza arubaini mume wangu akiwa hata hajanipigia simu kuniulizia hali yangu. Kweli nilichanganyikiwa, Mama aliniambia niende kutetea ndoa yangu, ingawa sikutaka lakini sikua na namna. Nilifika na siku hiyo nilimkuta mume wangu, hakunisemesha, baada tu ya kuniona alikasirika, lakini hakuondoka, alikaa pale na kuanza kunituma tuma. Angalau nilifurahi kidogo ananisemesha.

Bado hakua akihudumia hivyo nilijihudumia mwenyewe. Nikiwa katika kipindi hiki kigumu ndiyo nilifanikiwa kuona ukursa wako, nakumbuka ilikua ni mwaka jana mwezi wa nane mwishoni. Nilishakata tamaa ya maisha lakini post zako zilinifariji, nakumbuka nilikupigia simu na kukuomba ushauri, baada ya kuongea sana uliniambia nisome Kitabu chako, niache kulalamika, kukubali yaliyotokea na kuanza upya.

Kwangu ilikua ngumu, nilikuambia kabisa siwezi kumuacha mume wangu kwani sijui kama nitaenda wapi, nakumbuka uliniambia huo ni uamuzi wangu lakini kubaki haimaanishi kuvumilia bali kuendelea na maisha na kaucha kukumbatia maumivu. Uliniambia nisome Kitabu chako cha “Ndoa Yangu Furaha Yangu” kweli nilikisoma na niseme tu namshukuru Mungu kwani kilinisaidia sana.

Katika kipindi hicho ndiyo ukatoa Kitabu chako cha Biashara 50, kwakua kile cha kwanza kilinisaidia niliamua kukinunua. Sikujutia kwani ilinipa moyo sana, biashara ambazo mwanzo niliona kama za kijinga siwezi kufanya uliziandika na kuonyesha namna ya kufanikiwa katika hizo biashara. Kwakua sikua na mtaji mkubwa basi nilianza na biashara ya Diamond Karanga.

Kila siku nilikua nikipeleka ofisini na kuziuza kwa wafanyakazi wenzangu, nilianza hivyo na kweli nilikua napata faida kwani siku box moja lilikua linaisha hivyo kupata hata elfu kumi, nilikua nauzia pia nyumbani. Baada ya kuona nafanikiwa nilitaka sana kufungua sehemu ya kushona nguo, kweli naweza kushona lakini nilitaka kusimamia tu. Nilitafuta mafundi wanafunzi na kuwaambia nawaajiri.

Kupitia mtaji wa Diamond Karanga faida niliyopata nilinunua vyarahani vitatu na vifaa vingine, palepale nnje nyumbani nikaweka na kuanza kufanya hiyo kazi. Niliacha kabisa kumfuatilia mume wangu, sikua nalalamika tena, sikua naangalia simu yake na wala sikuruhusu aniguse kwani baada ya kuona simjali alitaka kunirudia, nikamuambia mpaka tupime kwanza kwani nina mtoto lazima niwe makini.

Alikasirika na kuwa hanigusi, lakini alipoona mambo yanaenda vizuri hasa katika kushona alianza kujileta na kujifanya kama ananipenda na nimsamehe, walianza kugombana na mchepuko wake kwani alikua anamsumbua sana kuhusu hela na yeye hakua na kitu. Sasa hivi yuko mbioni kutaka kunirudia lakini nimeshamuambia kuwa kama anautaka mwili wangu tena basi tukapime wote tena mara mbili.

Simuamini tena lakini najiamini, naamini nina thamani na nimeshamuambia kuwa sasa hivi siwezi kuvumilia tena manyanayso yake, sijlali tena kwani furaha yangu haimtegemei yeye, ninafuraha bila yeye. Ndoa yetu ni yakanisani, sitaki kuivunja lakini nimeshamuambia kuwa siwezi kuhatarisha maisha yangu , sipigwi tena na nilazima abadili tabia zake. Nashukuru sana kwani angalau sasa nina furaha, sijali kuhusu umri tena na najiamini.

***MWISHO



source https://utamuzaidiapp.blogspot.com/2020/05/simulizi-mume-wangu-alivyonisaliti-siku.html

No comments:

Post a Comment