MATARAJIO YA wengi katika uhusiano ni kuwa na furaha, hakuna kinachotafutwa katika mapenzi zaidi ya faraja ya moyo. Lakini ili uweze kuipata ni lazima kuwe na mapenzi ya dhati.
Vichwa vya wengi walio katika uhusiano ni kusaka penzi la dhati! Hakuna anayependa kunyanyasika au kuwa na mashaka na mpenzi wake. Katika hili lazima uwe makini sana, maana unaweza kuwa katika uhusiano na mwenzi ambaye ‘yupoyupo’ tu na wala hana mpango wowote na wewe, lakini wewe ukawa hujui.
Kwa bahati mbaya sana, baadhi ya marafiki zangu, wanashindwa kuchuja pumba na nafaka kwa sababu wakati wanafanya uchaguzi hawakuzingatia vigezo.
Vijana wengi wa siku hizi, huzingatia zaidi mwonekano wa nje, jambo ambalo ni baya kwani mwonekano wa nje, hauwezi kukuonesha mabaya ya mpenzi wako hata siku moja.
Kama ulichagua mwezi kwa kuzingatia tabia na mambo mengine ya msingi, ni rahisi zaidi kwako kugundua penzi ulilonalo ni la dhati au lile la ‘nataka pochi lako tu!’
Pointi ya msingi hapa ni lugha zenye ishara mbaya kwa wapenzi. Umewahi kujiuliza kuhusu hili? Umewahi kutafakari juu ya kauli chafu anazotoa mpenzi wako dhidi yako?
Yaani unashangaa mwenzi wako anakuwa mtu wa kutoa kauli za maudhi, kashfa na hata matusi wakati mwingine. Wewe unazichukuliaje? Rafiki zangu, kauli ya mtu inaweza kukutoa gizani na kugundua ukweli uliopo ndani yake, lakini kama hutakuwa makini, unaweza kuchukulia kama utani na kuuacha ukweli uendelee, mwisho unakuja kushtuka, umeshaachwa!
Hapa nimekuandalia kauli zenye ishara mbaya ya penzi lako. Ukiona moja kati ya kauli zifuatazo, basi kuwa na mashaka, kisha fanyia kazi, utagundua ukweli. HUVUTII!
Kati ya kauli mbaya zaidi katika uhusiano ni pale mpenzi wako atakapokuambia huna mvuto! Haijalishi amekuambia akiwa katika hali gani; utani au akimaanisha, lakini neno hilo si zuri kuambiwa na mpenzi wako.
Kuambiwa huvutii, katika mapenzi ni tusi kubwa. Nini maana ya mvuto basi? Nani umvutie? Ni wapita njia? Ofisini? Sokoni? Ana maana gani hasa?...
Siku zote mvuto ni kwa ajili ya mpenzi wako, ndiyo maana mkawa katika uhusiano, hii inamaananisha ulimvutia ndiyo sababu akakukubali. Kukuambia huvutii si utani, ni kweli haoni mvuto na inawezekana penzi limeshachuja.
Inawezekana akawa anafanya mzaha, kama ndivyo, atasoma ulivyopokea, akiona umekasirika atarekebisha usemi wake haraka, kama ni vinginevyo ataendelea kushikilia msimamo wake, hata kama ni kwa utani, lakini atakuwa anakufikishia ujumbe wako kwamba huna mvuto, kwa maneno mengine humvutii, humfai; kwa hiyo muachane. Kuna nini tena hapo? Akili kichwani mwako.
HUPENDEZI!
Hii ni kauli nyingine mbaya. Unapoambiwa: “Hujapendeza kabisa, yaani huna uwezo wa kupangilia nguo, kila siku unachemsha!” ujue kuna hatari hapo, angalia mara mbili uhusiano wenu.
Kuambiwa hujapendeza kunashusha thamani yako na kuonekana huna ujanja wa kufanya uchaguzi mzuri wa mavazi. Huenda ni kweli hujapendeza, lakini hilo si la kubeza.
Anatakiwa kukuambia kwa upole namna ambavyo unatakiwa kuvaa na kuonekana nadhifu. Kwa maneno mengine, kukuambia hujapendeza ni kama anakusuta, hakukubali na unamuaibisha!
Rafiki yangu mpenzi, bado kuna mengi ya kujifunza zaidi lakini kutokana na ufinyu wa nafasi yangu, naomba niweke kituo kikubwa hapa.
source https://utamuzaidiapp.blogspot.com/2020/05/hiz-hapa-ni-kauli-zenye-ishara-mbaya.html
No comments:
Post a Comment