Habari ya asubuhi mdau wa Opera News, tunatumai u bukheri wa afya.
Karibu katika dawati la dondoo tupate kukujuza habari tatu zinazoshika vichwa vya habari nchini asubuhi ya leo.
Zinazobamba leo ni pamoja na MBowe & TBC wayamaliza, ajitoa ubunge Hai kuunga mkono juhudi na mwisho ni juu ya JPM kumpoza Chenge
MBOWE & TBC WAYAMALIZA
Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) pamoja na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) vimeafikiana kufanya kazi kwa pamoja pasipo uhasama ili kuhakikisha umma wa Watanzania unapata habari pasipo vikwazo vya aina yoyote.
Makubaliano hayo yamefikiwa leo katika kikao cha pamoja cha usuluhishi kilichoongozwa na Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Dkt. Charles Mahera, chini ya uratibu wa Jukwa la wahariri Tanzania (TEF).
Kufuatia makubaliano hayo, TBC itaendelea kuripoti matukio mbalimbali ya mikutano ya kampeni ya CHADEMA pamoja na shughuli nyingine za chama hicho, kama inavyofanya kwenye vyama vingine vya siasa.
Dkt. Mahera amevitaka vyama vya siasa na wafuasi wake kutoa ushirikiano kwa vyombo vya habari badala ya kupandikiza chuki na kusababisha vishindwe kutekeleza majukumu yake ya msingi wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu zinazoendelea nchini.
AJITOA UBUNGE HAI
MGOMBEA ubunge wa Hai mkoani Kilimanjaro kwa tiketi ya Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Ibrahim Simbo, ametangaza kujitoa katika kinyang’anyiro hicho kwa kile alichodai kumuunga mkono mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli.
Simbo alitangaza uamuzi huo juzi mbele ya waandishi wa habari, akidai kuwa ameona atajichosha bure kushindana na kutumia nguvu nyingi ilhali ana nafasi nzuri ya kumuunga mkono mgombea urais kwa tiketi ya CCM kwa kuwa kazi zake zinaonekana waziwazi.
Wagombea ubunge wanaoendelea na kampeni zao katika Jimbo la Hai ni Saashisha Mafuwe (CCM), Mbarouk Mhina (ACT-Wazalendo) na Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe.
JPM AMPOZA
MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. John Magufuli amemweleza aliyekuwa mbunge wa Bariadi Mkoa wa Simiyu, Andrew Chenge, kuwa asiwe na wasiwasi kwa kukosa ubunge kwani bado kuna vyeo vingi serikalini.
Amesema hayo jana, Agosti 4, 2020, wakati akiendelea na kampeni za kuwania nafasi hiyo na kuwatambulisha madiwani na wabunge wa chama hicho katika mji wa Bariadi kwa ajili ya uchaguzi mkuu ambao utafanyika Oktoba 28, mwaka huu.
“Nimezungumza Shinyanga na maeneo mengine, kazi zipo nyingi, Mzee Chenge ‘Mtemi’ ni kaka yangu kwelikweli, nilipoingia bungeni kwa mara ya kwanza mwaka 1995 mke wangu alikuwa na mimba, aliyenisaidia pesa za kwenda hospitali ni Chenge. Huu ndiyo ukweli,” alisema na kuongeza:
“Mheshimiwa Chenge kazi zipo nyingi mno hata utemi nao ni kazi kubwa tu. Bariadi achaneni na maneo ya upinzani, leo nataka niwaite wote watatu; Andrew Chenge (Bariadi), Dkt. Chegeni (Busega) na Salum Mbuzi (Meatu) waniombee kura hapa. Njooni hapa wote.
source http://www.bongoleo.com/2020/09/05/dondoo-za-leo-mbowe-wayamaliza-ajitoa-ubunge-hai-jpm-ampoza/
No comments:
Post a Comment