Wednesday, September 16, 2020

Dondoo za leo; Lissu afukua makaburi/ Awashiwa moto/Alilia kodi za utalii

Habari yako mdau wa Opera News, tunatumai u Bukheri wa Afya

Karibu kwenye dawati la dondoo tupate kukujuza habari tatu zinazoshika vichwa vya habari nchini siku ya leo.

Zinazobamba ni pamoja leo ni pamoja na Lissu kufukua makaburi, Membe kuwashiwa moto na Lema alilia kodi za utalii. Karibu;

AFUKUA MAKABURI

TUNDU Lissu, mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) amesema, ugomvi wa wakulima na wafugaji ‘ni la kuundwa.’

Kwenye mkutano wake wa kampeni za rais Mbarali, Lissu amesema, maeneo yenye migogoro awali yalikuwa ni mashamba ya wananchi, kisha yakachukuliwa na serikali na baadaye yakakabidhiwa wawekezaji ambao nao badala ya kulima, wanayakodisha.

“Ukienda Mkoa wa Morogoro Wilaya ya Mvomero, Kilosa na Kilombero, hizo wilaya tatu za Morogoro ndio kitovu cha migogoro ya wakulima na wafugaji. Sasa imehamia Mbarali mkoa wa Mbeya.”

“Ukiemda Bonde la Rufiji sasa kuna migogoro ya wakulima na wafugaji, ukienda Rukwa kwenye Hifadhi ya Katavi sasa kuna migogoro ya wakulima na wafugaji.”

MEMBE AWASHIWA MOTO

Mbunge Mteule wa Viti Maalum Wanawake Mkoa wa Dodoma kupitia CCM, Mariam Ditopile amemvaa mgombea Urais kupitia ACT-Wazalendo, Benard Membe kuwa iwapo atashinda urais atautumia kusafiri nje ya nchi kwa maslahi yake binafsi kwa kigezo cha kutibiwa.

” Nimemsikia akisema alienda Dubai kwa ajili ya kuchekiwa afya yake, hii inashangaza Nchi yetu imepiga hatua kubwa sana kwenye sekta ya Afya, tuna Vituo vya Afya kila mahali, Hospitali za Wilaya za kutosha, Hospitali kubwa kila kanda zenye vifaa vya kisasa leo mtu anaenda kucheki afya nje ya nchi na hajawa Rais akipewa nchi si ndo atahamia kabisa?

Rais Magufuli amejitahidi kusitisha safari za nje zisizo na ulazima, yeye mwenye hajawahi kwenda kuchekiwa afya nje ya nchi achilia mbali kutibiwa, Membe yeye kwenda kupima homa tu anaenda Dubai, hii imewaonesha watanzania kuwa yeye ni kiongozi wa aina gani na hakika watamkataa kwa kishindo Oktoba 28,” Amesema Mariam Ditopile.

ALIA NA KODI ZA UTALII

MGOMBEA ubunge Arusha Mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Godbless Lema, amesema chama hicho kikipewa ridhaa ya kuongoza nchi, kitafuta utitiri wa kodi, ambao ni tatizo katika sekta ya utalii.

Akizungumza jana katika mkutano wake wa nane wa kampeni katika viwanja vya Soko la Kilombero jijini hapa, Lema alisema katika sekta ya utalii kuna zaidi ya kodi 36, ambazo ni kikwazo kikubwa kwa watalii, hivyo chama hicho kikishika dola kitafuta baadhi ya kodi zisizostahili kuwapo.

Akizungumza juzi katika moja ya mikutano ya kampeni jijini hapa, Lema alisema Tanzania ni moja ya nchi duniani zenye vivutio vingi vya utalii, lakini pato lake haliendani na vivutio vilivyopo.

“Tanzania ina vivutio vingi vya utalii, lakini pato la utalii na idadi ya watalii, haviendani na vivutio vilivyopo,” alisema Lema huku akibainisha kuwa kwa mwaka Tanzania inapokea watalii milioni moja tu na idadi hiyo inachagizwa na wingi wa kodi kwenye sekta hiyo.



source http://www.bongoleo.com/2020/09/17/dondoo-za-leo-lissu-afukua-makaburi-awashiwa-moto-alilia-kodi-za-utalii/

No comments:

Post a Comment