Wednesday, September 23, 2020

Dondoo za leo; Lissu aomba kura za kimbunga/ Ajinyonga, aacha tuhuma/ Viongozi 28 ACT wakamatwa

Habari yako mdau wa Opera News, tunatumai u Bukheri wa Afya

Karibu kwenye dawati la dondoo tupate kukujuza habari tatu zinazoshika vichwa vya habari nchini siku ya leo.

Zinazobamba ni pamoja na pamoja na Lissu kuomba kura za kimbunga, ajinyonga na kuacha tuhuma kwa mkewe na mwisho ni juu ya viongozi 28 wa ACT wakamatwa. Karibu;

AOMBA USHINDI WA KIMBUNGA

MGOMBEA urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, amewaomba wananchi kumpigia kura nyingi ili apate ushindi wa kimbunga katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, mwaka huu.

Lissu aliomba kura hizo jana alipokuwa kwenye mkutano wake wa kampeni eneo la Kamachumu wilayani Muleba mkoani Kagera, akiwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura siku hiyo, ili ushindi wa CHADEMA uwe wa kimbunga.

“Tukishinda kidogo, wataiba, tukishinda kawaida wataiba! Ili wasiibe, inabidi tushinde kwa kimbunga ili wakose kwa kuanzia, wakute kila kituo cha kuhesabia kura, katika jimbo, wilaya, mkoa tumeshinda,” alisema.

Aliwataka wananchi wafanye kile alichokiita kurudisha mapigo kwa kuipigia kura CHADEMA, akitamba kuwa kwa kufanya hivyo, wapinzani wao watakuwa wamepigwa kwa namna ambayo hawatainuka tena.

“Mwezi ujao tuzuie hili balaa tupige kura tujikomboe, tarehe 28 mwezi Oktoba iwe ni siku mpya,” Lissu alisema.

UGOMVI wa mume na mke ndani ya nyumba, umemalizika baada ya mwanaume kuamua kujiua na kuacha waraka wenye tuhuma dhidi ya mkewe.

Edward Chakala ni mume wa mtu, mkazi wa Kata ya Ilembo mkoani Katavi, ambaye ameamua kujinyonga hadi kufa, huku akimtuhumu mkewe, Pendo Elia kumtelekeza katika mazingira magumu.

AJIUA  NA KUACHA TUHUMA KWA MKEWE

Kwa mujibu wa familia ya Chakala, ndugu yao huyo alifikia hatua hiyo ya kujitoa uhai kwa kutumia chandarua chumbani kwake, huku akiacha waraka kuwa chanzo cha yeye kuchukua uamuzi huo mgumu, ni kufuatia kutelekezwa na mkewe.

Akisimulia sababu ya tukio hilo baya kuwahi kutokea kwenye familia yao, dada wa marehemu, Janeth Chakala alisema kuwa, kaka yake alijinyonga baada ya mke wake kumkimbia.

“Kaka yangu aliugua sana, ndipo mke wake akamkataa na kumkimbia kwa sababu hakuwa na uwezo wowote.

“Kwa hiyo, kaka yangu alikuwa anakwazika na maudhi ya mkewe, na mara nyingi alikuwa akimbembeleza sana arejee nyumbani hadi ikafikia hatua akamnyang’anya watoto, lakini bado mke wake hakumkubali,” anasema Janeth kwa uchungu.

VIONGOZI 28 WAKAMATWA

VIONGOZI na wanachama 28 wa Chama cha ACT-Wazalendo Mkoa wa Kaskazini Pemba, Zanzibar wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kujeruhi na kuwafanyia fujo wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani humo.

Taarifa  hiyo imetolewa Jana Jumatano tarehe 23 Septemba 2020 na, Juma Sadi Khamis, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba wakati akizungumza na MwanaHALISI Online.

Kamanda Khamis amesema, watu sita walikamatwa kwa tuhuma za kuchora nyuma za wanachama wa CCM huku 22 wakikamatwa kwa tuhuma za kuhusika na tukio la kujeruhi wanachama watatu wa CCM katika Msikiti wa Kandagani visiwani humo.

“Kulikuwa na matukio ya kuchorwa baadhi ya majumba  yanayolengwa ya CCM, baada ya kupata taarifa hiyo, tulifanya operesheni kuanza kuwatafuta wanaohusika, tuliwakamata watu sita na tunaendelea nao na utaratibu wa kesi,” amesema Kamanda Khamis.

Kamanda Khamis amesema “baada ya hilo, ikatokea tukio la kushambuliwa msikiti na kupigwa wanachama wa CCM tukio limetokea  alfajiri ya jana Jumanne tarehe 22 Septemba 2020, tumeanza opereshehni  na watu 22 tumewashikilia.”



source http://www.bongoleo.com/2020/09/24/dondoo-za-leo-lissu-aomba-kura-za-kimbunga-ajinyonga-aacha-tuhuma-viongozi-28-act-wakamatwa/

No comments:

Post a Comment