Wednesday, November 27, 2019

Shahidi Aeleza Mahakama Adhabu Ilivyosababisha Ulemavu Wa Mgongo Kwa Mwanafunzi

Kesi ya jinai inayomkabili Mwalimu Focus Mbilinyi , dhidi ya Jamhuri kwa tuhuma za kumpiga Mwanafunzi na kumsababishia ulemavu, imeendelea kusikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wilaya ya Njombe, ambapo mashahidi wawili wa upande wa Jamhuri wamefika mahakamani hapo kuwasilisha ushahidi wao.

Kesi hiyo namba 141 ya mwaka 2019, inayomkabili aliyekuwa Mwalimu wa Shule ya Msingi Madeke, Focus Mbilinyi, imeendelea kusikilizwa mahakamani hapo chini ya Hakimu Irvan Msaki na Wakili wa Serikali Elizabeth Malya.

Shahidi wa Kwanza Given Nyanginywa, ameiambia Mahakama kwamba mnamo tarehe 21 March, Mwalimu Focus Mbilinyi, alitoa Hesabu 10 na baadae alitoa adhabu kwa wanafunzi wote waliokosa na miongoni mwa walioadhibiwa siku hiyo ni pamoja na Hosea Manga, ambaye alipigwa viboko 10 huku akiwa amening’inizwa dirishani kwa mtindo wa miguu juu kichwa chini, ambapo baada ya Hosea kupigwa viboko hivyo, alianguka chini na kushindwa kunyanyuka.

Kwa Upande wake shahidi namba 4 Daktari Silvery Mwesige, ameiambia Mahakama kwamba, Mtoto Hosea Manga walimpokea takribani wiki mbili, baada ya kupata matatizo akitokea Hospitali ya Ikonda.

Ameiambia Mahakama pia baada ya vipimo kufanyika walibaini kuwepo kwa mgandamizo chini ya uti wa mgongo, uliopelekea kupishana kwa pingili za uti wa mgongo na kusababisha mfumo wa damu kushindwa kupenya kwenda sehemu za chini za mwili wa mtoto huyo.

Licha ushahidi huo kuwasilishwa mahakamani hapo pamoja na kielelezo cha Ripoti ya Matibabu ya mtoto huyo, mawakili upande wa utetezi walipinga kielelezo hicho kwa madai ya kwamba, ripoti hiyo ya matibabu imewasilishwa na mtu ambaye hajaiandaa, pingamizi ambalo Mahakama imelitupilia mbali.

Kesi hiyo imesikilizwa kwa zaidi ya masaa sita,  ambapo baadaye Mahakama ilikikubali kielelezo hicho kilichowasilishwa na Daktari silvery Mwesige, kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, kitengo cha mifupa MOI, na kesi hiyo imeahirishwa hadi Desemba 2, 2019.

Kesi hiyo ni ya pili kufunguliwa kwa tukio lililomkuta mtoto Hosea Manga.

Kesi ya awali namba 83 ya mwaka 2017 ilifutwa kutokana na daktari aliyemtibu kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili kushindwa kufika mahakamani kutoa ushahidi licha ya kuitwa mara nane.

No comments:

Post a Comment