Karani wa Mahakama ya Wilaya ya Temeke, Itialy Omary, amefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam kwa madai ya kuomba rushwa ya Sh. 200,000.
Mshtakiwa huyo alisomewa mashtaka yake mbele ya Hakimu Mkazi Agustina Mmbando.
Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Odessa Horombe, alidai kuwa mshtakiwa huyo anakabiliwa na shtaka la kupokea rushwa kinyume cha sheria.
Horombe alidai kuwa Aprili 27, 2018 katika viunga vya Mahakama ya Wilaya ya Temeke, mshtakiwa aliomba rushwa ya Sh. 200,000 kutoka kwa Musa Abdallah, ikiwa ni kishawishi cha kumsaidia kukwepa hatia dhidi ya shtaka lililokuwa linamkabili kesi namba 211/2018 ya usalama barabarani iliyopo mahakamani hapo. Mshtakiwa huyo alikana mashtaka hayo.
Horombe alidai kuwa upelelezi umekamilika na kuiomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kumsomea maelezo ya awali.
Hakimu Mbando alisema mshtakiwa anatakiwa kuwa na mdhamini mmoja mwenye vitambulisho vinavyotambulika na atasaini hati ya dhamana ya Sh. milioni tano.
Alisema kesi hiyo itasikilizwa maelezo ya awali Novemba 28, mwaka huu. Mshtakiwa alitimiza masharti hayo na yupo nje kwa dhamana.
No comments:
Post a Comment