Friday, November 29, 2019

ACT- Wazalendo wataka vifurushi bima ya NHIF Visitishwe, Serkali Yawajibu

Chama cha ACT Wazalendo kimeitaka Serikali kusitisha vifurushi  vya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Tanzania (NHIF) kwa madai kuwa vinakandamiza wasiokuwa na uwezo.

Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dorothy Semu, alipozungumza na waandishi wa habari.

Vifurushi hivyo vilizinduliwa juzi jijini Dar es Salaam na uongozi wa NHIF, ukieleza kuwa vimegawanywa katika makundi matatu yaliyopewa majina ya 'Ninajali Afya', 'Wekeza Afya' na 'Timiza Afya'.

Kwa mujibu wa mpango huo mpya wa matibabu wa NHIF, watu wenye umri wa kati ya miaka 18 na 35 watalipia Sh192,000 kwa mwaka kuwa katika kifurushi cha Najali Afya Premium ama Sh384,000 cha Wekeza Afya ama Sh516,000 cha Timiza Afya.

Kwa wenye umri mkubwa zaidi wa kuanzia miaka 36 hadi 59 watagharimia matibabu ya mwaka mzima kwa kulipia Sh240,000 katika mpango wa Najali Afya Premium au Sh444,000 (Wekeza Afya) au Sh612,000 (Timiza Afya).

Watu wenye umri wa kuanzia miaka 60 na kuendelea wataweza kugharimia matibabu ya mwaka kwa kulipia kati ya Sh360,000 na Sh984,000. Bei za vifurushi hivyo inaongezeka kulingana na idadi ya wanufaika kama mwenza na watoto hadi wanne.

Dorothy Semu alisema  kuwa kitendo cha serikali kujiondoa kwenye kuhudumia raia wake kwenye afya kwa kutangaza vifurushi vipya vya bima, ni kuwatenga wenye kipato cha chini.

Alisema gharama zilizowekwa katika vifurushi hivyo vipya zinajenga matabaka mawili katika utolewaji wa huduma za afya; la wenye nacho na wasio nacho.

“Binadamu hachagui kuumwa au aina ya ugonjwa ambao unapaswa kuugua, utaratibu huu wa vifurushi unachukulia kwamba suala la ugonjwa ni jambo la hiari, kwamba mtu anaweza kuchagua kuumwa ugonjwa huu ama kuukataa ule, hivyo atatibiwa kutokana na chaguo lake.

"Mtazamo wa namna hii ni hatari sana katika ujenzi wa jamii yenye utu, usawa na yenye haki. Duniani kote kuna bima aina mbili, ya binafsi na ya umma. Kiwango cha malipo ya kila mwaka kwa kila mtu ni tofauti kulingana na vigezo tofauti.

"NHIF kimsingi ni skimu ya bima ya afya ya umma, na kwa maana hiyo viwango vya malipo vinatokana na uwiano wa kipato cha mtu na mafao yanapaswa kuwa sawa kwa watu wote bila kujali kiasi cha mchango wanaotoa.

"Kitendo cha kutoa vifurushi vya malipo tofauti, na huduma kutolewa kwa kuzingatia kifurushi, ni kitendo cha kuifanya NHIF kuwa bima binafsi na 'kubidhaisha' afya ya Watanzania," alidai.


Chama hicho kilishauri kusimamishwa kwa huduma ya vifurushi hivyo vipya ili kupunguza matumizi makubwa ya rasilimali fedha.

“Kwa mfano, badala ya kuzuia wananchi wa kipato cha chini kupata huduma mbalimbali kama MRI na CT scan, serikali itoe ruzuku kwa wananchi hao kwa kuwalipia NHIF. Huu ndiyo wajibu wa serikali kutokana na kodi inazokusanya kutoka kwa wananchi,” alisema.


Hata hivyo, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu ameyajibu madai ya ACT- Wazalendo kwa kusema kuwa   Vifurushi hivi ni kupitia utaratibu wa HIYARI  na sio lazima. Pia, havijafuta Bima ya Afya ya Jamii (CHF) .

"Tusifanye siasa kwenye hili.  Vifurushi hivi ni kupitia utaratibu wa HIYARI sio lazima. Pili, havijafuta Bima ya Afya ya Jamii (CHF) ambapo kiwango cha kuchangia kwa mwaka ni shilingi 30,000 kwa kaya ya hadi watu 6. Aidha, vifurushi vya watoto, Wakulima nk. bado vipo." Ameandika Ummy Mwalimu katika ukurasa wake wa Twitter wakati akipangua Hoja ya Zitto Kabwe

No comments:

Post a Comment