UNAPOWASIKILIZA wanaume wengi wakizungumzia kile wanachodhani wao kinawagusa wanawake kwenye mahusiano, utashangaa orodha ya vitu hutawala mazungumzo. Kwa mwanaume wa kawaida, mwanamke anahitaji vitu ili akupende. Utasikia, "Ah, mwanamke pesa. Ukiwa na hela zako bwana, basi." Imani ni kwamba wanawake wanahitaji sana vitu na hivyo ndivyo vinavyowavuta na kuwabakiza kwenye mahusiano.
Pamoja na ukweli fulani kwamba vitu navyo vina nafasi yake kwenye mahusiano, hasa kwenye kizazi hiki cha sasa kinachotanguliza thamani ya fedha kuliko kitu kingine chochote, bado huwezi kuthamanisha moyo wa mwanamke na fedha, ingawa ni kweli anazihitaji. Kudhani kwamba baada ya kuhakikisha mwanamke amepata kila anachokihitaji kwa maana ya vitu, basi unaweza kuendelea na shughuli nyingine kwa kuamini umemaliza kazi, ni kutokuelewa mahitaji halisi ya kihisia ya mwanamke.
Najua wapo wanawake wasiohitaji kingine chochote kwa mwanaume zaidi ya fedha na vitu. Mahitaji ya kihisia tunayoyazungumzia wanajua wanakoyapata wao. Hawa si sehemu ya mjadala wetu leo. Tunachokizungumza sisi si uhusiano wa kibiashara kati ya watu wawili bali uhusiano wa watu hao wasiotaka kuona anajitokeza mtu wa tatu kuingilia mahitaji yao ya kihisia.
Shauku ya mwanamke: Constant affection
Hakuna kitu muhimu katika maisha ya mwanamke kama kujua anapendwa na kuthaminiwa kwa dhati na mpenzi wake. Kuthaminiwa kunafanya ajisikie kushiba ajabu. Na mwanamme yeyote anayeelewa umuhimu wa mahusiano na anayetaka kuukamata vilivyo moyo wa mke wake, basi anawajibika kuonyesha namna anavyovutiwa, anavyomkubali na kumthamini mke wake. Hiyo ndiyo gharama ya kuingia kwenye mahusiano.
Ni vizuri kuelewa ego ya mwanamke hujengwa na mwanamme na ikijengwa humfanya awe na amani na uhuru wa kufungua moyo wake na hivyo kuwa tayari kusikiliza, kuelekezwa na hata kufuata upepo wowote anaoutaka mume wake. Mengineyo yote yanayobaki, iwe fedha, nyumba, gari na kadhalika, ni mambo ya ziada tu na umuhimu wake unategemea sana namna alivyoshiba upendo wa mumewe. Bila kujisikia kupendwa na kuthaminiwa, yote hayo hayamzuii kupuuza na kuusitisha uhusiano.
Kusema hivyo hatusemi uchumi si suala la msingi kwa mwanamke. Wanawake wengi hujenga mahusiano na wanaume wenye msimamo au uelekeo fulani wa kiuchumi. Maana hakuna mtu anapenda kulala njaa. Ulofa haukubaliki. Lakini tunachokisema hapa ni kwamba kupendwa na kujaliwa ndio msingi.
Ili kumfanya mwanamke ajisikie kuvutia, kukubaliwa na kupendwa, mwanamme analazimika kufanya jitihada za makusudi kabisa, tena kila siku, kusema na kuyarudia maneno yanayothibitisha upendo alionao kwa mkewe.
Tunasema analazimika kwa sababu kiasili mwanaume hana hitaji la kuthibitishiwa anapendwa na hivyo wakati mwingine hudhani na kwa mke mambo ni yale yale. Kumbe pamoja na kuwa anajua anapendwa, bado mwanamke anatamani kusikia anapendwa kila wakati.
Lugha ya maneno na vitendo inayothibitisha upendo wa mume kwa mkewe haichoshi katika masikio ya mwanamke. Angependa kusikia siku zote, jinsi alivyo mzuri. Jinsi anavyopendeza. Jinsi anavyojua kupika. Jinsi anavyojua kuvaa. Jinsi alivyo mama mwema wa watoto na kadhalika. Mwenzi wako ameshinda salon masaa nane akitengeneza nywele, anaporudi nyumbani anatarajia uone alivyopendeza. Ni hitaji linalohitaji sensitivity. Ni zoezi endelevu lisilosubiri kuulizwa, "hivi nimependeza mume wangu?", "hivi bado mume wangu unanipenda?" Ni zoezi la tena na tena na tena. Ndio maana tunasema kuingia kwenye mahusiano yasiyotarajiwa kuwa ya mchepuko kuna gharama zake. Ni suala la mwanaume kujikana nafsi yako.
Sasa mambo gani yanapofanywa na mwanamme huonyesha affection kwa mke wake, hiyo hutegemeana na mwanamke alivyolelewa, imani yake, mazingira na haiba yake kama mwanamke.
Wapo wanawake wanaopenda kuandikiwa ujumbe wa maneno mazuri kwa wakati wasiotarajia. Wanataka kuambiwa wanavyomisiwa. Wengine wanapenda kukumbatiwa, busu, kushikwa mkono hadharani. Kwa jinsi hiyo wanajisikia karibu na wapenzi wao. Wengine wanapenda kutoka na waume zao mara kwa kwa mara, kulala sehemu nyingine mara moja moja, kutazama televisheni au filamu pamoja, kula pamoja, kuoga pamoja, kufunguliwa mlango wa gari wanapoingia. Wengine wanapenda wanaume wanaotumia muda wa kutosha na familia.
Ni vyema basi, mwanaume anayejua gharama ya uhusiano atafiti kujua ni kitu gani hasa kikifanywa huufanya moyo wa mke wake kuruka kwa furaha. Akifanya hivyo atakuwa amewekeza katika mahusiano yake, jambo ambalo ni la msingi kwa mwanaume yeyote asiyependa michepuko.
Umempa mkeo kipaumbele?
Pamoja na kuonyeshwa kwamba anapendwa kwa vitendo na maneno, mwanamke pia hutamani kujisikia yu katika mikono salama inayomjali na kumpa nafasi ya kwanza moyoni. Hakuna mwanamke angetamani kuwa kwenye mazingira ambayo anajikuta anashindania nafasi ya kwanza na kitu kingine chochote iwe ni kazi, majukumu mengine au mtu mwingine yeyote. Mwanamke hutamani kushika nafasi ya kwanza katika vipaumbele vya mume wake na sio kuwa ziada.
Nikupe mfano kulielezea hili. Chukulia umeahidiana na mwenzi wako, awe mke au mchumba, kukutana muda fulani mahali. Mwanamke anatarajia uwepo mahali hapo mlipokubaliana kwa wakati. Ikiwezekana anapokuja akukute ukimsubiri. Ukifanya hivyo, anajisikia fahari kwamba umeweza kuacha vyote ulivyokuwa ukivifanya kwa ajili yake. Unapata alama za ziada.
Sasa ni kawaida kwa wanaume wasiojali kuchelewa miadi. Mmekubaliana kukutana saa 10:00 wewe unafika saa 10:30 na hata ikibidi saa 11:00. Wakati mwingine mwanaume anayafanya haya kwa makusudi tu, ili asionekane anavyobabaika kumridhisha mwanamke. Lakini ni ukweli kwamba hali hii, ikigeuka kuwa tabia, inakupunguzia alama muhimu kwa mwanamke. Anakuona ni mtu usiyejali, usiyethamini miadi na usiyeaminika.
Kadhalika, mume au mwanaume asiyeweza kuwa na undivided attention kwa mwenzi wake anajikosesha alama za ushindi. Kuongea huku ukiendelea kutumia simu ukichat na marafiki wengine mtandaoni, ni kumfanya mke ajione hathaminiki na hana value; mume asiyeweza ku-concentrate kwenye mazungumzo kwa ujumla hufanya kosa la jinai kwa mwanamke. Maana mwanamke angependa kuwa na muda wa mazungumzo usioingiliwa na chochote.
Angalia mfano huu. Mke anayetamani kuwa muda wa faragha wa mazungumzo na mume wake anamwomba mumewe watoke kidogo wakapunge upepo baharini. Kutoka huko kuna maana kubwa kwake, kwamba ana nafasi katika ratiba ya mwenzi wake. Lakini jioni hiyo hiyo, mume wake anakumbuka ana kikao cha harusi ya rafiki yake ambacho, kwa maoni yake, hawezi kueleweka akikikosa.
Bila kufikiri umuhimu wa ombi la mkewe, mwanaume anaomba kirahisi tu wangeahirisha mtoko ili aweze kuhudhuria kikao cha harusi na safari ya baharini ipangwe siku nyingine. Katika mazingira kama haya, wanamke wengi hujisikia vibaya kuona hisia zao hazithaminiwi na hivyo wamefanywa kuwa 'ziada' au mengineyo katika ratiba za mwanamme. Jambo hili linaloweza kuonekana dogo, linaweza kabisa kuvuruga kabisa moyo wa mke hata kama hatasema wazi.
Ukitazama vizuri mahusiano utaona, mara nyingi, vipaumbele vya mwanaume katika ndoa huwa si vipaumbele halisi vya mwanamke. Wakati mwanaume akidhani mambo yanaenda kama kawaida, na ndoa inaendelea kuchanua, mke huweza kuwa na maoni tofauti kabisa kwa sababu ya matarajio makubwa moyoni mwake ambayo mara nyingine si rahisi kuyasema kwa uwazi na kwa urahisi.
Kumbe ilivyo ni kwamba mambo yanayougusa moyo wa mwanamke ni yale yanayoonekana kuwa madogo, lakini yenye umuhimu mkubwa kihisia. Kumbe mambo yanayoonekana kuwa ni ya kitoto fulani hivi kwa mwanaume, ndiyo mambo ya msingi kabisa katika kujenga hisia za mwanamke. Yasipotimizwa hayo, hata kama mahitaji mengine yanayoonekana kuwa makubwa yatatimizwa, hayatakuwa na maana yoyote.
'mapenzi ya kigumu' ni ubinafsi
Ni bahati mbaya sana katika utamaduni wetu wa ki-Swahili, wanaume hukuzwa kuamini kuwa ni jambo la aibu na fedheha kumwonyesha mwanamke mapenzi ya wazi. Tumekuzwa kuamini stahili ya mwanamke ni 'mapenzi ya kigumu' na kibabe. Tumeambiwa, "...mwanamke hapaswi kujua unampenda, tena mweke mwanamke mbali kabisa na wewe...asijue mambo yako mengi!"
Naweza kuuelewa msingi wa hofu hii katika utamaduni wetu wa kuendesha mambo yetu karibu yote kimya kimya na kwa siri siri. Lakini naelewa pia kuwa wanaume hawa hawa wenye kuyaamini haya na wenye mapenzi ya kibabe kwa wake zao, huwa tayari kuonyesha mapenzi ya kimahaba wanapojenga mahusiano mapya! Hiyo ni kumaanisha kuwa, pamoja na utamaduni wa kibabe, bado, inawezekana kabisa kuwa na mahaba na mke. Ni suala la uamuzi.
Kosa tunalolifanya wanaume wengi ni ubinafsi wetu wa asili. Tunaingia kwenye mahusiano kwa sababu za kufaidi na sio kulipa gharama ya faida inayotarajiwa. Hatuwekezi na tunataka gawio. Tunakuwa na mapenzi wa kigumu na kibabe tukisingizia shughuli nyingi za kutafuta maisha, hali inayotuweka mbali kihisia na wake zetu.
Tunaukumbuka ukaribu na mahaba pale tunapokuwa na shida ya 'chakula cha usiku'. Kufanya hivi, kwa kweli humfanya mwanamke ajisikie kutumika kama kifaa cha manufaa binafsi ya mume. Hili ni kosa la jinai kwa mwanamke. Mwanamke angehitaji affection ya kutosha isiyo na malengo ya kuishia kwenye 'chakula cha usiku'. Kila tendo la kimapenzi kwa mwanamke, sawa na fedha unazoweka benki, linakuongezea salio unaloweza kulipata baadae ukilihitaji. Ndivyo ilivyo unapohusiana na mwanamke. Weka akiba ya mapenzi, utapewa heshima unayoitaka.
Sasa mapenzi ya kigumu na kibabe tuliyoyazoea mara nyingi humfanya ashindwe kujiamini, ajihisi mpweke na mkiwa na hivyo bila kujua, hujikuta akijenga ukuta wa kimawasiliano kati ya moyo wake na mumewe. Matokeo yake, ule ukaribu uliotarajiwa kati yake na mume huanza kupungua kidogo kidogo, kuanzia moyoni, na hatimaye anaweza kujikuta akishindwa kumpa mumewe heshima na thamani inayostahili. Tutafafanua suala hili mbeleni.
Hivyo tunaweza kusema, mwanamme anapoanza kuona mabadiliko yoyote ya mahusiano na mke wake, pengine ni muhimu kujitazama na kuona ikiwa yeye mwenyewe hajaacha kufanya jukumu lake kwa kumfanya mkewe aamini bado anayo nafasi ya kwanza katika maisha yake.
Ahh, makala ndefu tena
Ila jiulize, umefanya nini kinachomfanya ajisikie kupendwa na kuthaminiwa? Umelipa gharama ya heshima na mamlaka unayoyadai kwenye mahusiano? Au unadhani fedha ni jibu la mambo yote? Fikiri upya.